Na Munir Shemweta, MANYARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinashirikisha wadau wa sekta mbalimbali wakati wa utekelezaji Mpango Kabambe katika maeneo yao.
Aidha, alitaka mipango kina inayoandaliwa katika halmashauri za Miji na Majiji kuhakikisha inazingatia mipango kabambe inayoandaliwa ili kuifanya miji kuwa na taswira nzuri.
Dkt Mabula alieleza hayo leo tarehe 12 Agosti 2021 wilayani Babati mkoa wa Manyara wakati akizindua Mpango Kabambe wa Mji wa Babati akiwa katika ziara yake ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara.
Alisema, ni vizuri watendaji wa halmashauri kuhakikisha wakati wa utekelezaji mipango kabambe wanashirikisha wadau kama vile sekta za maji, barabara na umeme na kusisitiza kuwa hawatakiwi kwenda kinyume na yaliyowekwa katika mpango huo ili kuifanya miji kuwa na taswira nzuri na inayovutia.
Naibu Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, Wizara yake inaendelea kuhamasisha uandaaji mipango kabambe kwenye maeneo mengine nchini ili kuongeza kasi ya upimaji pamoja na kuifanya miji kuwa katika sura nzuri.
"Kikubwa utekelezaji uzingatie mpango na lazima uwekwe wazi kwa kushirikisha wadau na kumkabidhi kila mdau kipande chake cha utekelezaji mfano barabara TANROAD au TARURA akabidhiwe, umeme TANESCO na maji wapewe mamlaka ya maji na utekelezaji uzingatie mpango usiende kinyume" alisema Dkt Mabula
"Unakuta barabra nzuri halafu anakuja mtu wa maji anapitisha mabomba yake na anaharibu kabisa na hapa lengo ni kuona miji yote inapangwa vizuri" Naibu Waziri Mabula.
Aidha, Dkt Mabula aliuelezea mpango kabambe aliouzindua kama njia mojawapo ya kutoa fursa za ajira sambamba na kuongeza kasi ya upimaji na hivyo kupunguza ama kuondoa migogoro ya ardhi.
Alizitaka Halmashauri ambazo bado hazijandaa mipango kabambe kuiga mfano wa halmashauri ya mji wa Babati kwa kuandaa mipango kabambe ili kuchangia shughuli za kiuchumi na kuagiza ofisi za mikoa na wilaya kufuatilia na kupatiwa ripoti ya utekelezaji Mpango Kabambe katika halmashauri husika ili kuleta maendeleo ya kichumi na kimazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Imaculata Senje alisema lengo la serikali katika uandaaji mpango kabambe ni kuona kasi ya upangaji inaoongezeka.
Kwa mujibu wa Bi. Senje, hadi sasa jumla ya mipango Kabambe 30 imeandaliwa kwenye makao makuu ya wilaya nchini na kusisitiza kuwa mipango hiyo inapoandaliwa hushirikisha sekta zote muhimu kama vile barabara, maji, umeme nk.
"Mipango unapoandaliwa inazingatia miradi ya kutekelezwa inayogusa sekta zote na ndiyo maana wakati wa uandaaji tunashirikisha sekta zote na gharama zinazoainishwa katika mpango ni kwa ajili ya miaka ishirini .
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizindua Mpango Kabambe wa Mji wa Babati akizindua Mpango Kabambe wa Mji wa Babati alipokuwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara tarehe 12 Agosti 2021. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Abdalaham Kololi na Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Imaculata Senje.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Abdalaham Kololi (Kulia) wakimkabidhi Nakala ya Mpango Kabambe wa Mji wa Babati Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji huo Bw. Daniel Luther wakati wa uzinduzi wa mpango huo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara tarehe 12 Agosti 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara tarehe 12 Agosti 2021. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Abdalaham Kololi.
Baadhi ya maafisa kutoka wizara ya ardhi na taasisi nyingine wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula alipokuwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara tarehe 12 Agosti 2021.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Imaculata Senje akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji wa Babati mkoani Manyara tarehe 12 Agosti 2021.
Sehemu ya watendaji wa Sekta ya Ardhi mkoa wa Manyara wakiwa katika kikao na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokuwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Manyara tarehe 12 Agosti 2021.
0 Comments