NA JUMA ISSIHAKA
INAWEZEKANA Watanzania wanaishia kusikia jina Stiegler’s Gorge hadi kuwa JNHPP bila kufahamu safari iliyofikisha majina hayo hadi sasa ambapo wanatarajia neema ya Megawati lukuki za umeme zitakazozalishwa kutokana na mradi huo.
Hakuna shaka kwamba Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umekuwa kiungo muhimu katika safari ya mafanikio yaliyofikiwa na yanayotarajiwa, hiyo ni kutokana na Wataalamu wake kutoka Taasisi ya Ushauri wa Kihandisi ya TANROADS (TECU), kuwa ndiyo Mshauri Mwelekezi wa mradi huo.
Hatua hiyo ni ishara nzuri kwa taifa ambapo awali, ajira za namna hiyo zilitolewa kwa kampuni za nje ya nchi na hivyo kuwaacha vijana bila shughuli za kufanya.
Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo TANROADS kupitia Kampuni yake tanzu ya TECU inasimamia, pia imani hiyo kwao imetokana na ithibati ya weledi usio kifani ulioonyeshwa nao katika kazi ilizowahi kuzisimamia.
Hatua hiyo pia ni muhimu na bora zaidi kutokana na kwamba fedha inayolipwa haipotei na badala yake inabaki katika mzunguko wa ndani na hivyo taifa linajiimarisha na taasisi zake.
Kadhalika, hatua hiyo imepigia mstari ukweli kwamba Tanzania inao wataalamu wenye uwezo wa kufanya kazi yoyote, mahali popote tena kwa uaminifu na weledi mkubwa, hili linathibitika kwa TECU.
Ikumbukwe kuwa katika mradi huo asilimia 64 ya wafanyakazi ni Watanzania na hadi sasa haijaripotiwa kupotea kwa kifaa chochote, huo ni uthibitisho wa uaminifu wa Watanzania na uzalendo waliyonao.
Pia, mradi huo unasimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ikiwa ni wawakilishi wa serikali kuhakikisha Mkandarasi anatekeleza kazi zote kwa mujibu wa Mkataba.
CHIMBUKO LA STIEGLE’S GORGE
Stiegler’s Gorge si jina geni masikioni mwa Watanzania, kutokana na ukweli kwamba, limekuwa likihusishwa na masuala ya nishati ya umeme kwa takribani miongo minne hadi sasa.
Hata hivyo, ufahamu wa jina hilo haumaanishi utambuzi wa asili yake ndani ya Bonde la Mto Rufiji, kwani chimbuko lake ni mpelelezi mmoja raia wa Uswisi aliyefahamika kwa jina la Stiegler.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Tanzania The Limits to Development from Above, kilichoandikwa na Kjell Havnevik, asili ya jina hilo ni tukio la mwaka 1907, ambapo mpelelezi huyo Stiegler alikanyagwa na tembo hadi kufariki dunia.
Inaelezwa kuwa, mpelelezi huyo akiwa katika shughuli za uwindaji ndani ya Pori la Akiba la Selous, alivamiwa na tembo na kuuawa kisha mwili wake kusukumwa mpaka kwenye maporomoko ya maji yaliyopo katika eneo la Mto Rufiji.
Hata hivyo, vyanzo vingine vinabainisha kuwa, Stiegler hakuuawa na tembo, bali alianguka kwa bahati mbaya ndani ya bonde hilo na kupoteza maisha.
Kwa ujumla simulizi ya kifo cha Stiegler katika eneo hilo la maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ndiyo iliyozaa jina la Stiegler’s Gorge.
Mtandao wa Kimataifa wa Africantourer unaelezea Bonde la Stiegler’s Gorge kuwa linafanana kwa ukaribu na lile la Canyon la nchini Marekani.
Africantourer unabainisha kuwa, Stiegler’s Gorge ni sehemu ya Mto Rufiji ndani ya Pori la Akiba la Selous lenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000 na lilipitishwa kuwa moja ya sehemu yenye urithi wa dunia mwaka 1982.
Eneo hilo linatajwa kama ‘mpalio mwembamba’ wenye urefu wa kilomita nane, upana wa mita 50 na kina kutoka kilele chake cha maji ni mita 100.
UTAFITI WA RUBADA
Utafiti uliofanywa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980 na Shirika la Kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) kwa kushirikiana na kampuni ya kigeni ya M/s Norplan/Hafslund, ulionyesha kuwa mradi wa Stiegler’s Gorge una uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme mwingi wa maji (hydro-power) zaidi ya umeme ambao Tanzania inahitaji.
Matokeo ya utafiti huo pia yalionyesha kuwa mpalio wa Stiegler’s Gorge una uwezo wa kuhimili mitambo mitatu mikubwa ya kuzalisha umeme.
Mtambo wa kwanza ukizalisha megawati 400 ambao ungefungwa upande wa Kaskazini mwa Bwawa, mtambo wa pili ungekuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 800, ambao ungefungwa upande wa chini ya bwawa, na mtambo wa tatu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 900 ambao ungefungwa upande wa kusini mwa bwawa.
Kwa ufupi, jumla ya megawati 2,100 zingezalishwa kutoka Stiegler’s Gorge, kiasi ambacho ni karibu ya mara mbili ya kinachohitajiwa
….FAIDA YA STIEGLER’S GORGE
Leo hii linapotajwa jina la Stiegler’s Gorge, fikra za Watanzania zinajielekeza kwenye faida moja tu ambayo ni ukombozi wa uchumi wa taifa hili.
Faida hiyo si nyingine, bali ni nishati ya umeme. Kama ambavyo Rais Dkt. John Magufuli, amesimama imara kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwenye bonde hilo, ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.
Kusudio hilo si geni, bali ni mwendelezo wa kutimiza dhamira ambayo aliiweka Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, takribani miongo minne iliyopita ambaye aliwaza kujenga bwawa hilo ili kuisaidia nchi kupata umeme wa kutosha.
Stiegler’s Gorge, ambayo kwa mujibu wa taarifa ya satellite inapatikana umbali wa kilomita 185 kutoka jijini Dar es Salaam, kwa sasa inaangaliwa kama kitovu kitarajiwa cha kuimarisha mzizi mkuu wa uchumi wa nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kama mradi huo utakamilika utazalisha umeme maradufu ya unaozalishwa sasa na mazingira hayo yatasaidia kupatikana umeme wa uhakika kwa nchi nzima.
Kwa muktadha huo, dhamira ya sasa ya Rais Dkt. Magufuli inakusudia kuwapo kwa nishati ya umeme inayojitosheleza ili kukidhi dira ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ambao ni muhimili mkubwa wa lengo la nchi kukua kiuchumi.
Katika kutimiza dhamira ya mradi wa uzalishaji mkubwa wa umeme kutoka kwenye Bonde la Stiegler’s Gorge, Rais Dkt. Magufuli alisisitiza umuhimu wa kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye eneo hilo ambapo sasa linashuhudiwa likitekelezwa kupitia Kampuni za kizalendo kwa kushirikiana na waandishi kutoka Bara la Afrika.
Julai Mosi mwaka 2017, wakati akifungua maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Rais aliwaeleza wawekezaji kuwa changamoto ya umeme wa uhakika itakwisha, kwa sababu Tanzania itakuwa na umeme wa megawati kati ya 4,000 na 5,000 pindi mradi wa Stiegler’s Gorge utakapokamilika.
“Mvua inyeshe ama jua liwake, nitatekeleza mradi huu mkubwa ambao umeshindikana kwa zaidi ya miaka 40 baada ya kuwekewa vikwazo mbalimbali,” kauli ya Dkt. Magtufuli mwaka 2017.
Udadisi usio wa kina zaidi wa gazeti hili, unaonyesha kuwa, chimbuko la wazo la kuwa na mradi wa Stiegler’s Gorge lilipata nguvu zaidi mwaka 1975, wakati Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipoyapambanua mawazo yake juu ya umuhimu wa kuwa na mradi mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme katika bonde hilo.
Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huo ulipata vikwazo vingi, hususan vya uharibifu wa mazingira, ambavyo viliibuka kila panapokaribia hatua nzuri, tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza mpaka ulipofika wa Rais Dkt. Magufuli ambaye amefanikiwa kuutekeleza.
Ukimwacha Mwalimu Nyerere, wamepita marais wengine ambao ni Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Dkt. Jakaya Kikwete, wote kwa sababu hizo na nyingine walikumbana na vikwazo vya utekelezaji huo.
Ikumbukwe matumaini ya Watanzania ya kupata umeme wa bei nafuu wa maji wa Stiegler’s Gorge yalipata msukumo mpya, mwezi Septemba, mwaka 2011 wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, Bernard Membe, na maofisa kadhaa wa Tanzania, walipokwenda Sao Paolo, nchini Brazil kufanya mazungumzo na wenzao wa huko kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kuisaidia Tanzania katika mradi huo.
Waliporejea nchini, umma ukatangaziwa kuwa mradi wa umeme wa maji wa Stiegler’s Gorge utaanza karibuni na utatekelezwa na wataalamu kutoka Brazil.
Umma ukaambiwa pia ifikapo mwaka 2015 Watanzania wataanza kuufaidi umeme wa bei rahisi wa Stiegler’s Gorge.
Hata hivyo, mpaka utawala wa awamu ya nne unaondoka madarakani matumaini hayo hayakutimia kama ilivyoahidiwa.
….MAAMUZI MAGUMU YA JPM VS WAPINZANI WA KIMATAIFA KUHUSU UTEKELEZAJI WA STIEGLER’S GORGE
Katika kile kinachoitwa dhamira ya Rais Dkt. Magufuli ya kutekeleza wazo hilo la Mwalimu Nyerere, Juni 28 mwaka 2017 alikutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.
Ikumbukwe kuwa, Ethiopia ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotajwa kufanikiwa kuzalisha umeme mwingi unaozidi megawati 60,000 kutoka vyanzo mbalimbali kama maji, upepo, jua na joto ardhini.
Katika maelezo yake, Rais Magufuli alisema mradi huo utakaozalisha umeme wa megawati takribani 2,100 utatekelezwa kwa fedha za ndani, ambazo alisema zipo na kwamba upembuzi yakinifu umekwishafanyika.
Anasema anafahamu zipo kelele nyingi za watu watakaohoji fedha za ujenzi zitakakopatikana, lakini atatekeleza mradi huo na endapo atapata wafadhili wenye masharti nafuu ataungana nao.
Anasema mradi huo ukikamilika, ikichanganywa na megawati 1,460 zinazozalishwa sasa na megawati 600 zinazozalishwa kutoka miradi ya Kinyerezi I, II, III, nchi itaweza kuzalisha megawati 4,000 hadi 5,000.
UPINZANI WA KIMATAIFA
Ni vyema tukajikumbusha serikali ilipoweka bayana ujenzi wa mradi huo kuwa utaathiri asilimia tatu tu ya Pori la Akiba la Selous, baadhi ya mashirika ya kimataifa yaliibuka na misimamo yao ya kupinga mradi huo kwa hofu ya uharibifu wa mazingira.
Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyama Pori la (WWF), katika andiko lake la mwaka 2017 lilifafanua kuwa, ujenzi wa mradi huo ungesababisha uharibifu wa mazingira ya Mto Rufiji kuelekea Bahari ya Hindi.
Maelezo ya WWF yalijikita katika msisitizo kwamba, uharibifu huo utagusa moja kwa moja ardhi ya eneo hilo na maeneo mengine ya pori na kusababisha momonyoko wa ardhi kiasi cha tani milioni 16.6 kwa mwaka.
Kadhalika, ilibainishwa kuwa kutakuwapo na madhara ya kemikali zitokanazo na shughuli zitakazofanyika katika eneo hilo na zaidi mtazamo huo ulijikita katika tishio la kutokea mmomonyoko mkubwa wa ardhi, kuibuka kwa maziwa, pia hali na kuvurugwa muundo wa delta ya Rufiji.
Rais Dkt. Magufuli, aliwahi kuweka bayana kuhusu vikwazo vya kimazingira kwa kusema hawezi kusikiliza kelele za watu wa mazingira kwa sababu ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kuhifadhi mazingira, tofauti na inavyoelezwa.
“Mbuga ya Wanyama ya Selous ipo Tanzania na wenye maamuzi ya kuchimba bwawa la kuzalisha umeme ama laa ni sisi,” alisema Dkt. Magufuli mwaka 2017.
Jina la JNHPP limetoka wapi?
Septemba 6 mwaka 2018, Rais Dkt. Magufuli, wakati wa uzinduzi wa Ujenzi wa Barabara ya kilometa 51, inayoanzia Makutano (Butiama) - Natta hadi Mugumu, mkoani Mara, alibainisha kuwa ni vyema mradi huo upewe jina la kizalendo.
Alipendekeza badala ya kuitwa Stiegler’s Gorge, bora uitwe Kambarage Gorge ama Mwitongo Gorge na hilo ndiyo chimbuko la jina la Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP).
Kwa sasa kabla ya kukamilika kwa mradi huo, Tanzania kupitia vyanzo mbalimbali inazalisha megawati 1,602.32 za umeme kutoka megawati 1,308 za mwaka 2015 na kufanya nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020/25, kiasi hicho kinachozalishwa kinakidhi mahitaji na kufanya nchi kuwa na ziada ya umeme ambao ni megawati 445, ukilinganisha na mahitaji ya sasa ambayo ni megawati 1,120.12.
Ilani hiyo inafafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano hii, Chama kitaielekeza serikali kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa mradi wa JNHPP na kuanza kuzalisha wa megawati 2,115 za umeme.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Arab Contructors na JV Elsewedy Electric Wote kutokea nchini Misri chini ya Mshauri mwelekezi TECU kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
0 Comments