Naibu Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewatoa hofu wananchi wa Kata ya Ruhuhu
Wilaya ya Ludewa ambao wamekuwa wakiulalamikia ujenzi wa Daraja la Mto Ruhuhu
ambao umechukua muda mrefu kukamilika kwake.
Mhandisi Kasekenya ameyasema
hayo mkoani Njombe mara baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi wa kata
hiyo na kuelezwa kero na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi.
“Hili daraja ni la muda mrefu tangu mwaka 2016
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alikwisha
pita hapa na kuona adha na kero mnazozipata na alitoa ahadi kuwa lazima daraja
hili likamilike na ndio maana tuko hapa kukamilisha ahadi hiyo”, amesema Naibu
Waziri Kasekenya.
Aidha, amewaagiza Mameneja wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe na Ruvuma kuhakikisha ndani ya
wiki mbili kuanzia sasa vifaa vya ujenzi wa juu ya daraja vilivyopo Bandari ya
Dar es Salaam vifike eneo hilo na kuanza kufungwa ili wananchi wa kata hizi waanze
kutumia daraja.
Naibu Waziri Kasekenya ametoa
wito kwa wananchi kulilinda daraja hilo ambalo linagharimu kiasi cha shilingi
bilioni 6.1 pindi litakapokamilika kwani linajengwa kwa fedha za Serikali
kupitia kodi za wananchi.
“Kawaida daraja linapokamilika
wananchi wanaanza kuchimba mchanga, kuiba vyuma vya daraja na kupitisha mifugo
mahali pasipotakiwa, hivyo niwaombe wananchi mlilinde sana daraja hili”,
amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Kasekenya amekagua ujenzi wa barabara ya Itoni – Ludewa - Manda (km
211.4) sehemu ya Lusitu - Mawengi (km 50) kwa kiwango cha zege ambao
unatekelezwa na Mkandarasi Cheon Kwang Engineering Costruction na ujenzi wake
umefikia asilimia 69.
“Tunaendelea kumshukuru na
kumpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea tena kwa kasi,”
amefafanua Naibu Waziri Kasekenya.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa
barabara hii ya Itoni – Ludewa - Manda kutafungua fursa za kiuchumi kwa mkoa wa
Njombe na Tanzania kwa ujumla kwani maeneo hayo ndipo yanapopatikana kwa wingi
makaa ya mawe na chuma cha liganga.
Kwa upande wake Kaimu Meneja
wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua, amemueleza Naibu
Waziri huyo kuwa kazi zilizofanyika
mpaka sasa ni ujenzi wa tabaka la zege kwa kilometa 30, ujenzi wa makalvati
makubwa 11 na makalvati madogo 96 kati
ya 107 yamekamilika na kazi zingine
zinaendelea.
Naye, Mbunge wa Jimbo la
Ludewa, Joseph Kamonga amemshukuru Naibu Waziri kasekenya kwa kuweza kukagua na
kutembelea miradi iliyopo jimboni kwake na pia ameishukuru Serikali chini Rais
Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo mkoani Njombe kwa
wakati na wakandarasi wote wapo maeneo yao ya kazi.
Imetolewa na Kitengo Cha
Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
0 Comments