Na Faraja Mpina, TARIME
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ameendelea kutoa elimu juu ya manufaa ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi katika ziara yake ya kikazi ambapo mpaka sasa amezuru katika Mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dodoma, Geita, Kagera, Mwanza na Mara pamoja na Wilaya zake na kuhamasisha utekelezaji wa Mfumo huo katika ngazi ya halmashauri za Wilaya na Manispaa zote nchini
Amesema kuwa katika ziara zake amefurahishwa kuona baadhi ya Halmashauri wanaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka katika makusanyo yao ya ndani huku akizitolea mfano Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Mwanza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Nyamagana kwa juhudi walizozionesha katika kutekeleza Mfumo huo
Akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Tarime na Rorya Mkoani Mara Mhandisi Kundo amefanya mazungumzo na kamati za ulinzi na Usalama za Wilaya hizo na kuelezea kwa kina umuhimu wa Mfumo huo kuwa utazisaidia sana halmashauri katika kuwabainisha walipa kodi na kuweza kukadiria makusanyo ya halmashauri kwa kila mwaka wa fedha
Ameongeza kuwa Mfumo huo utasaidia taasisi za Serikali kama vile jeshi la polisi, zimamoto, na wataalam wa afya kufika kwa urahisi na kuchukua hatua katika maeneo yenye dharura za uhalifu, wahamiaji haramu, majanga ya moto, dharura za ugonjwa au ajali kwa kufuata taarifa za jina la barabara au mtaa na namba ya nyumba ambayo itakuwa imetolewa na mtoa taarifa
Mhandisi Kundo amezungumzia Mfumo huo kuwa unakwenda kurahisisha kufanyika kwa biashara mtandao kwa sababu una taarifa za kila eneo kama vile barabara, mitaa namba za majengo na makazi ya watu hivyo kurahisisha mfanyabiashara kumfiki8a mteja wake mahali alipo kwa kufuata vibao vinavyoonesha majina ya barabara, mtaa na namba ya nyumba au jengo husika
Aidha Mhandisi Kundo amesema kuwa taarifa zote zinakuwa zimehifadhiwa katika kanzidata ambapo mtu yeyote akitaka kuzitumia atazipata kupitia Programu Tumizi ya ya simu za mkononi ya NAPA ambayo itampatia mhusika ramani ya kufika pale anapotaka kufika kwa kuingiza taarifa za mtaa au barabara na namba za nyumba au jengo husika
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo kukamilika kwake kutachochea kukua kwa uchumi wa dijitali kupitia biashara mtandao lakini pia ni Mfumo muhimu sana kwa usalama wa nchi yetu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) vibao vinavyoonesha majina ya barabara katika Manispaa ya Musoma ikiwa ni moja ya miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unaotekelezwa chini ya Wizara hiyo kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara vya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) wakati akikagua vibao vinavyoonesha majina ya barabara katika Manispaa ya Musoma ikiwa ni moja ya miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unaotekelezwa chini ya Wizara hiyo kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara vya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akionesha mahali ambapo kibao cha pili kwenye nguzo inayoonesha majina ya barabara ilipotakiwa kukaa wakati akikagua miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi katika Manispaa ya Musoma. Aliyegusa nguzo ni Mtendaji wa Wizara Peter Mwita akigusa mahali ambapo kibao cha pili cha “SOKONI RD” kilipotakiwa kuwekwa
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kulia) akizungumza na Meneja wa TTCL Mkoa wa Mara Charles Msoma katika Ofisi za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) alipotembelea ofisi hiyo iliyopo Musoma.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akizungumza na watumishi wa Shirika la Mawasiliano (TTCL) alipotembelea Ofisi za Shirika hilo zilizopo Musoma Mkoani Mara
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kulia) akizungumza na Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Mara alipotembelea Ofisi hizo katika ziara yake ya kikazi katika Mkoa huo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye miwani katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Wizara, taasisi zake na makampuni ya simu, kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime na Watendaji wa Mpaka wa Sirari alipotembelea Mpaka huo kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya Mawasiliano.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa nne kulia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Juma Chikoka wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo wengine ni ujumbe alioambatana nao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo
0 Comments