Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF.SHEMDOE ATOA ONYO KWA WAKURUGENZI WANAOFICHA BARUA ZA UHAMISHO


Katibu Mkuu Prof Riziki Shemdoe akitoa maelekezo ya barua za Uhamisho wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya Msingi Nyahanga iliyopo katika Manispaa ya Kahama.

*******************************

Na Atley Kuni- KAHAMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Prof. Riziki Shemdoe amekemea vikali na kuonya tabia ya baadhi ya Wakurugenzi na watumishi wa Idara za Masjala wasio na weledi kuficha barua za uhamisho ambazo tayari zimesainiwa na Katibu Mkuu TAMISEMI, huku wakitengeneza mazingira ya viashiria vya rushwa ili waweze kukabidhi Barua hizo kwa wahusika.

Shemdoe amefikia azma hiyo wakati wa Ziara ya Kikazi wilayani Kahama mkoani Shinyanga iliyomalizika mwishoni mwa juma, ambapo kwa nyakati tofauti amesema amekuwa akipokea malalamiko yasiyo isha juu ya mkwamo huo wa baadhi ya Barua za Uhamisho kutokuwafikia watumishi waliopata uhamisho kwa kwa wakati.

"Kumeibuka wimbi la baadhi ya Wakurugenzi na Watumishi wa sehemu ya cha Masjala katika Ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa kushindwa kutoa barua ambazo tayari zimesainiwa na Katibu Mkuu TAMISEMI na kutumwa kwenye Halmashauri, kwaajili yakuwapa wahusika lakini watu wachache kwa matakwa yao wamekuwa wakikwamisha Barua kwenda kwa wahusika, hili halikubaliki na hii ni kwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma." ameonya Shemdoe.

Prof. Shemdoe alisema, kufuatia malalaamiko hayo, hivi sasa Ofisi ya Rais TAMISEMI, inaendelea kufuatilia ili kubaini wale wote wenye kuendekeza vitendo hivyo, aidha kwa kiongozi yeyote wa Halmashauri au mtumishi atakayebainika kufanya unyanyasaji huo, basi sheria itachukua mkondo wake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI hivi sasa zoezi la uhamisho linafanyika kila baada ya miezi mitatu na Barua zote za Uhamisho zinasainiwa na Katibu Mkuu TAMISEMI, mara baada ya muombaji kukamilisha hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na barua hizo kupitishwa na mamlaka zao za ajira na kuombewa vibali kwa Makatibu Tawala wa Mkoa kabla yakuwasilishwa TAMISEMI kwa hatua za mwisho za uhamisho.

Post a Comment

0 Comments