Viongozi mbalimbali wakiwa eneo la mradi wa ujenzi huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKANDARASI Gemen Engineering Company Ltd, anayejenga Daraja la Msingi lililopo Wilaya ya Mkalama mkoani Singida amesema daraja hilo litakabidhiwa rasmi Serikalini Oktoba 30 mwaka huu baada ya ujenzi wake kukamilika.
Hayo yalisemwa na Mhandisi wa ujenzi wa daraja hilo Method Mwalongo wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge katika ziara yake ya siku moja ya kukagua daraja hilo aliyoifanya jana.
"Mheshimiwa mkuu wa mkoa ujenzi wa daraja ili unaendelea vizuri na tunatarajia kulikabidhi serikalini Oktoba 30 mwaka huu,". alisema Mwalongo.
Akipokea taarifa ya ujenzi wa daraja hilo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge, aliwashukuru viongozi wa Wilaya ya Mkalama, Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Singida kwa ushiriki wao mkubwa wa ujenzi wa daraja hilo ambalo ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Dk. Mahenge alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo na kumtaka mkandarasi kumaliza haraka ujenzi kama alivyoahidi kabla ya mvua hazijaanza kunyesha.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja hilo Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Singida, Mhandisi Matari Masige alisema daraja hilo ambalo limegharimu Sh. 10.9 Bilioni ni kiungo muhimu kati ya Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu kupitia Barabara ya Mkoa ya Ulemo, Gumanga na Sibiti.
" Daraja hili pia ni kiungo muhimu kuunganisha makao makuu ya Wilaya ya Mkalama na Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, kupitia daraja la Sibiti, hadi Mkoa wa Mara," alisema Masige.
Masige alisema mradi huo ni ahadi ya Hayati Dk. John Magufuli, aliyekuwa Rais wa Tanzania aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema daraja hilo linajengwa takribani umbali wa meta 10 upande wa juu toka lilipo daraja la sasa likiwa na urefu wa meta 100 zilizogawanywa sawa katika sehemu nne zenye urefu wa meta 25 kila sehemu (spans).
Alisema daraja hilo lina jumla ya upana wa meta 10.2 zinazojumuhisha upana wa meta 7.6 ikiwa ni sehemu ya njia za kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja na sehemu iliyosanifiwa kupita kwa watembea kwa miguu yenye upana wa meta 1.3 kila upande.
" Ujenzi wa daraja hili pia unahusisha ujenzi wa barabara za maingilio (approach roads) kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 1 (yaani meta 300 upande wa Ulemo na meta 700 upande wa Gumanga) pamoja na kalvati moja lenye ukubwa wa meta 4x2.5 (upana x kimo) upande wa Ulemo".alisema Masige.
Alisema madhumuni ya daraja hilo ni pamoja na kuwaondelea wananchi kero ya usafiri wa barabara waliokuwa wanaipata kutokana na daraja la vyuma la zamani lililokuwa la muda (temporary) kuwa jembamba na ambalo pia nguzo zake zilititia kutokana na kuchimbwa na mkondo wa maji hivyo kuwa hatarishi kwa watumiaji wa barabara na wananchi kwa ujumla.
Aidha Masige alisema kuwa daraja hilo linajengwa kwa zege na litakuwa la kudumu zaidi ya miaka mia moja. Pia magari zaidi ya Tani 50 yatapita baada ya kukamilika daraja hili.
Alisema matarajio yao baada ya ujenzi kukamilika ni kuwa hali ya usafiri na usafirishaji kati ya Mkoa wa Singida na Mikoa ya kanda ya ziwa hasa Mkoa wa Simiyu na Mara itaboreka zaidi. Vilevile Wananchi wa Wilaya za Mkalama na Iramba wataboresha hali zao za uchumi kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa usafiri wakati wote.
Alitaja changamoto kuwa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2019 hadi mwezi Mei, 2020 sehemu kubwa ya kazi za daraja zilisimama kutokana mto kujaa maji hivyo kushindwa kuendelea na kazi, hata hivyo Mkandarasi aliendelea na kazi ya kuinua tuta la barabara kadri hali ya hewa ilivyoruhusu.
Alisema mategemeo yao baada ya mradi huo kukamilika wananchi wa pande zote zinazounganishwa na daraja hilo wataweza kusafiri na kusafirisha mazao yao kwa urahisi zaidi na hivyo kujiongezea kipato na kuinua uchumi wao na wa Taifa kwa Ujumla na vivile kutaunganisha Mkoa wa Singida na ukanda wa Ziwa kupitia daraja la Mto Sibiti ambalo tayari limekamilika.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo aliishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo litakuwa mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo ambao amewataka kuilinda miundombinu yake.
0 Comments