Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAKAMILISHA UJENZI MRADI WA MAJI WA SH. 192.7 MILIONI IKUNGI.

Wananchi wa Kijiji cha Dung'unyi wilayani Ikungi mkoani Singida wakichota maji jana baada ya Serikali kukamilisha mradi wa maji uliogharimu zaidi ya Sh.192.7 Milioni ambao utahudumia watu 4946 wa Vijiji vya Dung'unyi na Munkinya.
Mhandisi wa Maji Victor Kamate, akizungumza na wananchi wakati alipokuwa akikagua mradi huo.
Afisa Mtendaji Kata ya Dung'unyi, Yahaya Njiku, akimtwika maji Mmoja wa Wananchi wa Kijiji cha Dung'unyi.
Muonekano wa mradi huo wa maji.

 Tenki la kuhifadhia maji la mradi huo.



Na Dotto Mwaibale, Singida


SERIKALI imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wenye gharama ya zaidi ya Sh.192.7 Milioni uliotekelezwa katika Vijiji vya Dung'unyi na Munkinya wilayani Ikungi mkoani Singida.

Akizungumza na waandishi wa Hmhabari jana Afisa Mtendaji Kata ya Dung'unyi, Yahaya Njiku alisema kukamilika kwa mradi huo kutawaongezea kasi ya maendeleo wananchi wa vijiji hivyo ambao walikuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya kazi za uzalishaji.

Alisema mradi huo utawanufaisha wananchi zaidi 4946 wa vijiji hivyo ambao sasa wameondokana na adha waliyokuwa wakiipata ya kukosa maji.

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo Njiku alisema unahusisha tenki la maji lenye ujazo wa lita 50,000 ambalo limejengwa kwenye mnara wa mita 12. 

Alisema chanzo cha maji cha mradi huo ni kisima chenye uwezo wa kutoa 4,800 lita kwa saa, mtandao wa mabomba unaofikia kilomita 5.6 huku kukiwa na jumla ya vituo saba vya kutolea maji.

"Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi hivi sasa wameanza kupata huduma ya maji wakati tukisubiria uzinduzi wake rasmi,". alisema Njiku.

Njiku ameipongeza Serikali kwa kumaliza mradi huo kwa wakati na akatumia nafasi hiyo kumshukuru  Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Ikungi Mhandisi Hoppeness  Liundi kwa kuwashirikisha viongozi  wa Serikali na wananchi katika kutekeleza mradi huo ambao ni mmoja kati ya miradi mikubwa wilayani humo.

Njiku amewataka wananchi wa vijiji hivyo kulinda na kutunza miundombinu ya mradi huo na kumshukuru  Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za miradi katika wilaya hiyo.

Njiku ametoa onyo  kwa mtu yeyote atakaebainika anahujumu miundombinu ya mradi huo na kuwa  Serikali haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria.

Aidha Njiku amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Singida  Mashariki, Miraji Mtaturu kwa kuwasemea bungeni wananchi wa Kata ya Dung'unyi  jambo lililosaidia kupatikana kwa mradi huo katika vijiji hivyo na Kijiji cha  Kipumbuiko.

Wakazi wa vijiji hivyo wakiongea kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuwakamilishia mradi huo na kueleza kuwa walikuwa na changamoto kubwa ya maji  kwani walilazimika kwenda kuchota kwenye visima vya kienyeji  na madimbwi ya maji ya mvua.

Theresia Mghesi Mkazi  wa Kijiji cha Dung'unyi alisema wanawake ndio waliokuwa wakihangaika usiku na mchana kufuata maji umbali mrefu wa zaidi ya kilometa saba  hali iliyosababisha wakati mwingine ndoa zao  kutetereka.

Post a Comment

0 Comments