Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS YAENDELEA NA UTOAJI ELIMU KWA WATUMISHI WA UMMA KUHUSU MADHARA YA MATUMIZI YA BIDHAA HAFIFU

Afisa usalama wa chakula (TBS) Bw.Barnabas Jacob akitoa elimu kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu kwa watumishi wa TANESCO,TRA, TTCL, NIDA na Benki ya Biashara ya Posta (TCB). Elimu hiI itawawezesha watumishi hao kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii na familia zao kwa ujumla kupinga matumizi ya bidhaa hizo. Afisa usalama wa chakula (TBS) Bw.Barnabas Jacob akitoa elimu kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu kwa watumishi wa TANESCO,TRA, TTCL, NIDA na Benki ya Biashara ya Posta (TCB). Elimu hiI itawawezesha watumishi hao kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii na familia zao kwa ujumla kupinga matumizi ya bidhaa hizo. Watumishi wa TANESCO,TRA, TTCL, NIDA na Benki ya Biashara ya Posta (TCB) wakipata kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu kutoka kwa Afisa usalama wa chakula (TBS) Bw.Barnabas Jacob (hayupo pichani).




Na Mwandishi Wetu, Nachingwea


WATUMISHI wa umma katika taasisi mbalimbali wilayani Nachingwea mkoani Lindi, wamepatiwa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya bidhaa hafifu hususani vipodozi ambavyo vimekatazwa kutumika nchini kutokana na kuwa na viambata sumu.

Mafunzo hayo kwa watumishi wa umma wilayani Nachingwea yametolewa kwa siku mbili na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kuwawezesha kuwa mabalozi ndani ya jamii kwa kupinga matumizi ya bidhaa hafifu, hususani vipodozi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo, Afisa Usalama wa Chakula wa TBS, Barnabas Jacob alisema mbali na kuelimishwa madhara ya bidhaa hafifu za vipodozi na vyakula, lakini pia wameelimishwa kuhusiana na majukumu ya shirika hilo.

Kwa mujibu wa Jacob miongoni mwa watumishi waliopatiwa elimu hiyo ni wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya ya Posta (TPB), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na wale wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Jacob alifafanua kwamba elimu hiyo itawawezesha watumishi hao kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii na familia zao kwa ujumla.

"Kwa hiyo elimu hii imelenga taasisi za umma ikiwa ni mwendelezo wa shirika kutoa elimu kwa umma kuhusiana na madhara ya vipodozi na vyakula vilivyopigwa marufuku," alisema Jacob na kuongeza;

"Tumeona tukitoa elimu hii kwa watumishi wa umma ana kwa ana inaweza kuwasaidia moja kwa moja hadi kwenye familia zao,majirani ,jamii kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata vya sumu."

Alisema shirika haliwezi kushinda vita hiyo bila wananchi kupewa na elimu, ndiyo maana wameona wafike kwenye taasisi za umma ili kutoa elimu kwa watumishi kuhusu madhara ya kutumia bidhaa hafifu zilizokatazwa nchini zikiwemo za vipodozi na vyakula.

Kupitia mafunzo hayo watumishi hao wameelimishwa madhara ambayo mtu anapata iwapo anatumia vipodozi vyenye viambata sumu kwa muda mrefu.

Alitaja madhara makubwa ambayo anaweza kupata ni kuwashwa kwenye ngozi, kuvimba,ngozi kuharibika kuchanikachanika,madhara katika mfumo wa uzazi kwa mwanamke na hata kupelekea kupata kansa ya ngozi.

"Lakini viambata sumu vilivyomo kwenye vipodozi vilivyopigwa marufuku vinaweza kuingia ndani ya mwili na kuathiri viungo vya ndani, mfano maini, figo na wakati mwingine baadhi ya kemikali zinaweza zikaenda hadi kwenye mfumo wa uzazi kwa hiyo hayo madhara yanaenda hadi kwa watoto" alisema Jacob.

Alipoulizwa ni kwa jinsi gani watumishi hao walivyopokea mafunzo hayo, Jacob alisema wamefurahi sana na wameahidi kueneza elimu hiyo kwa familia zao, majirani na jamii kwa ujumla .

Wakati huo huo maofisa hao wa TBS wamefanya ukaguzi madukani kwa ajili ya kuondoa kwenye soko bidhaa zilizoisha muda wake na pamoja na zile zilizopigwa marufuku nchini.

"Tuna utaratibu wa kupita kwenye masoko kuangalia bidhaa na tukikuta zimeisha muda wake tunaziondoa na vipodozi vyenye viambata sumu tunavikamata na kuviondoa sokoni," alisema Jacob

Aidha, maofisi hao walitembelea wajasiriamali pamoja na wenye viwanda na kuzungumza nao katika maeneo yao ya biashara kwa lengo la kuwahamasisha wajitokeza TBS kupata alama ya ubora.

Alitoa wito kwa wajasiriamali na wenye viwanda wilayani Nachingwea kujitokeza TBS kwa ajili ya kupata alama ya ubora ambapo huduma hiyo hutolewa bure bila gharama zozote Kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kupitia Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo SIDO.

Post a Comment

0 Comments