Na Salome Majaliwa – Dar es Salaam
12/08/2021 Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kutoa huduma kwa wateja wanaowahudumia kwa kufuata maadili ya kazi na kuepuka mazingira ya rushwa kwa kufanya hivyo wananchi wataridhika na huduma wanazozitoa.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na wajumbe waliohudhuria kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI alisema ushirikiano wa pamoja baina ya wafanyakazi pamoja na uwazi katika utendaji kazi vinachangia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma bora kwa wateja wanaowahudumia wakiwemo wagonjwa.
"Unapomuhudumia mteja toa huduma yako kwa moyo na kujituma epuka kuchukuwa hela za mgonjwa sijasema kama mnafanya hivyo bali natoa onyo kwani yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu”,.
“Hakikisheni wateja mnaowahudumia wanaridhika na huduma mnayoitoa kwani kupata huduma ni haki yao na wewe unawajibika kutoa huduma hiyo kwani Serikali imekuajiri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi”, alisema Prof. Janabi. Mwenyekiti huyo wa baraza la wafanyakazi alisema menegimenti ya Taasisi hiyo itaendelea kusimamia na kuhakikisha wafanyakazi wanapata maslahi yao kwa wakati na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja wao wakiwemo wagonjwa.
Akitoa mada kuhusu majukumu na wajibu wa wajumbe wa baraza la wafanyakazi Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Kazi Deus Mshelila alisema ni muhimu kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi wakafahamu wajibu wao kwa kufanya hivyo kutasaidia baraza hilo kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wafanyakazi.
Alisema katika Taasisi yeyote ile ukitoa kikao cha Bodi kikao kinachofuata ni baraza la wafanyakazi hivyo basi kikao hicho ni cha muhimu kwani kinajadili na kushauri namna ya utekelezaji wa masuala ya Kisera na uchumi wa Taasisi.
"Katika kikao cha baraza la wafanyakazi hakuna kunyoosheana vidole bali ni kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na kushauri, kurekebisha na kukosoa kasoro zilizopo katika utendaji kazi kwa maslahi ya wafanyakazi na Taasisi husika”,.
“Kisheria vikao vya baraza la wafanyakazi vinafanyika mara mbili kwa mwaka lakini kama kuna jambo la dharula vinaweza kufanyika mara tatu kwa mwaka”, alisema Mshelila.
Kwa upande wake katibu wa baraza la kwanza ambaye amemaliza muda wake Dkt. Samweli Rweyemamu alishukuru kwa nafasi aliyopewa ya kufanya kazi katika baraza hilo na kuwaomba wajumbe na menejimenti ya Taasisi hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wapya waliochaguliwa.
Katika kikao hicho cha baraza la pili la wafanyakazi tangu ianzishe Taasisi hiyo mwaka 2016 ulifanyika uchaguzi wa kuchagua Katibu na Katibu msaidizi ambapo Afisa Tawala Abdulrahman Muya alichaguliwa kuwa Katibu na Afisa Uuguzi Theresia Marombe alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi
Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA Agnes Kuhenga akisoma bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala Idara ya Mipango kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam John Bosco Quman akikata utepe kuashiria uzinduzi wa baraza la pili la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi cheti cha shukrani Katibu Msaidizi wa baraza la wafanyakazi la kwanza ambaye amemaliza muda wake Renatha Miiruko wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza la pili la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi cheti cha shukrani Katibu wa baraza la wafanyakazi la kwanza aliyemaliza muda wake Dkt. Samweli Rweyemamu wakati wa kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Picha na JKCI
0 Comments