Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI BASHUNGWA AUAGIZA UONGOZI WA BAKITA KUTENGENEZA MIFUMO YA KIELEKRONIKI

 

***********************

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa ameuagiza uongozi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kutengeneza mifumo ya kielektroniki itakayomuwezesha mtu yeyote anayehitaji huduma ya mkalimani wa lugha na hasa lugha ya Kiswahili, kuipata huduma hiyo kwa njia ya mtandao na kwa haraka zaidi.


Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo Agosti 21 wakati akizindua vifaa vya ukalimani, katika hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika ofisi za BAKITA Jijini Dar es Salaam.


Waziri Bashungwa amesema, Serikali kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu, imetoa kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 187 kugharamia ununuzi wa vifaa hivyo, ikitarajia kuona mabadiliko chanya ya taaluma hiyo kwa manufaa ya wengi wenye uhitaji na kwa ajili ya uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.


“Ili kuenenda sawa na uwekezaji huu, nawaagiza BAKITA wekezeni nguvu kwenye kubuni mifumo ya kielekroniki itakayomuwezesha mtu kuomba na kupatiwa mkalimani kwa njia ya mtandao, hatuwezi kwenda kizamani zamani lazima twende kidigitali ndiyo maana halisi ya uwekezaji huu” amesema Waziri Bashungwa.


Aidha, Waziri Bashungwa amesema  Watanzania wote wanawajibika kuiendeleza zaidi lugha ya Kiswahili kwa kuwa Tanzania ndiyo chimbuko la lugha hiyo. Hivyo kama taifa, lina wajibu wa kuhakikisha wanaohitaji kujua Kiswahili wanapatiwa rasilimali mbalimbali zitakazowawezesha kukielewa na kukitumia kwa usanifu na ufasaha zaidi. 


Awali akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.  Pauline Gekul  amesisitiza matumizi na utunzaji mzuri wa vifaa hivyo ili kutimiza azma ya Serikali ya kuendeleza utaalamu wa ukalimani nchini.


Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi, amesema vifaa hivyo vilivyonunuliwa vina uwezo wa kuwezesha jumla ya lugha nane kufanyiwa ukalimani kwa wakati mmoja. 


Vifaa hivyo vinajumuisha chombo maalumu kwa ajili ya kuchagua lugha na kuzungumza, seva, vipaza sauti, visikizi, spika, kikuza sauti na mashine ya mkalimani, ambavyo vinaweza kutumiwa na watu thelathini kwa wakati mmoja. 

Post a Comment

0 Comments