Ticker

6/recent/ticker-posts

KIKWETE AIPONGEZA WIZARA YA SANAA, TAMADUNI NA MICHEZO KUTANGAZA VYANZO VYA UTALII BAGAMOYO


*********************** 

NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO 

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Wizara ya Sanaa,Tamaduni na Michezo kutumia tamasha la Bagamoyo kutangaza vyanzo vya Utalii vilivyopo wilayani Bagamoyo hasa historia ya Utumwa. 

Ametoa pongezi hizo hapo jana wakati akifunga rasmi Tamasha la Kimataifa la Utamaduni Bagamoyo lililofanyika kwa siku tatu katika Viwanja vya Chuo cha Taifa cha Sanaa na Utamaduni TASUBA Bagamoyo. 

Aidha amefurahi kuona wasanii wanatengenezewa mazingira bora zaidi ya kuhakiki na kudhibiti haki za kazi zao na kuhakikisha wanalipwa inavyostahiri. 

Alisema matumaini yake taasisi zote zinazosimamia sekta ya sanaa watafanya kazi kubwa ya kulinda kazi za wasanii ili sekta hiyo iweze kukua na kufika mbali kama matarajio yao. 

Dkt.Kikwete alisema sanaa sikuizi inalipa kuliko zamani,sanaa ni ajira na sikuizi wasanii wanashindana na kuweza kuhakikisha sanaa na hata michezo kukua. 

"Sanaa ni ajira, imeajiri watu wengi, zamani tulizoea kuona kuna Mbaraka Mwishehe,Dar Jazz,Sikinde,Kilwa Jazz lakini sasa hivi hata hauwezi kuhesabu idadi yake na inalipa". Alisema Mhe.Dkt.Kikwete. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa moyo Wizara kuendeleza Tamasha hilo lenye historia katika Taifa la Tanzania. 

“Kwa dhati kabisa nitumie fursa hii adhimu kumshukuru mama yetu, Mhe. Rais kwa kuona changamoto ya ufinyu wa bajeti unaoikabili Wizara yetu, hivi karibuni ameelekeza Wizara yetu na Wizara ya Fedha kukaa pamoja ili kufanyia kazi changamoto hii” aliongeza Mhe. Gekul. 

Alifafanua kuwa Tamasha hili ndiyo Tamasha kongwe zaidi nchini na limebeba historia ya Taasisi ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo. 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakar Kunenge ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa Tamasha hili ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara kuboresha tamasha hilo ambalo amesisitiza kuwa lina faida kubwa siyo tu kwa wakazi wa Bagamoyo bali kwa taifa zima. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Zainab Abdallah amemshukuru Dkt.Kikwete kuweza kufika katika tukio hilo pamoja na baadhi ya viongozi kuona umuhimu wa tamasha hilo na kuweza kufika kushiriki na wananchi wa Bagamoyo. 

Amemshukuru Katibu Mkuu wa UVCCM Bw.Kenani Kihongosi kwa kuweza kushiriki tukio hilo linalowagusa vijana wa nchi hii ambalo limekuwa la kihistoria kwa mafanikio makubwa. 

"Asanteni wote mliofanikisha tamasha la 40 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kuwa la mafanikio makubwa sana. Mwisho wa tamasha hili ni maandalizi ya tamasha lijalo". Alisema DC Zainab.

Post a Comment

0 Comments