Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUANDAA JUKWAA LA MFUMO WA KIDIGITALI KWAAJILI YA UCHAMBUZI WA HALI YA HEWA KUBAINI MADHARA YA MAFURIKO NA UKAME


Katibu Mkuu, Ofisi Ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana Na Wenye Ulemavu), Mhe. Tixon Nzunda akitoa akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa Oktoba 13, 2021.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

********************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Ili kuhakikisha tahadhari za maafa yanayotokana na hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa uhakika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaandaa jukwaa la mfumo wa kidigitaji kwa ajili ya uchambuzi wa hali hewa ili kubaini madhara ya mafuriko na ukame kwa wakati.

Ameyasema hayo leo Katibu Mkuu, Ofisi Ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana Na Wenye Ulemavu), Mhe. Tixon Nzunda akitoa taarifa Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa Oktoba 13, 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijjini Dar es Salaam, Mhe.Nzunda amesema Serikali imeandaa mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika halmashauri 20 zilizoonekana kuwa katika hatari kubwa ya kuathirika na maafa.

"Halmashauri zilizoandaliwa mipango ya dharura ni Chamwino, Kondoa na Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma; Shinyanga Vijijini na Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga; Bariadi, Maswa na Meatu katika Mkoa wa Simiyu); Mwanga na Same katika Mkoa wa Kilimanjaro; Kilosa, Mvomero na Kilombero katika Mkoa wa Morogoro; Mtwara Manispaa, Halmashauri ya Mtwara na Masasi katika Mkoa wa Mtwara; Bukoba Manispaa, Bukoba halmashauri katika mkoa wa Kagera; Meru katika Mkoa wa Arusha; na Liwale katika Mkoa wa Lindi". Amesema Mhe.Nzunda.

Mhe.Nzunda amesema Menejimenti ya maafa nchini inazingatia utaratibu wa uhusiano wa kisekta unaotoa ushiriki thabiti na utangamano na wadau wote. Majukumu ya utendaji yanazingatia taasisi yenye wajibu wa kisheria, ujuzi pamoja rasilimali zinazohitajika.

"Kila sekta inawajibika kutambua hatari za maafa katika eneo lake, kutenga rasilimali kabla ya tukio na kujenga uwezo wa kukabili kuanzia ngazi ya taifa, mikoa, wilaya, kata, kijiji na jamii. Majukumu ya jumla kwa makundi mbalimbali". Amesema Mhe.Nzunda.

Amesema Wizara, idara na taasisi zinapaswa kuongoza juhudi za kupunguza madhara ya maafa pamoja na kusimamia hatua za kukabiliana na dharura kwa kutumia rasilimali zake. Sekta zinapaswa kuchukua hatua za kuainisha majanga, kutathmini hatari, kufuatilia na kuchukua hatua kupitia mipango na bajeti zake.

Aidha amesema Sekretarieti za Mikoa zina jukumu la kuainisha vipaumbele vya kupunguza madhara ya maafa, kuandaa mikakati, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa masuala ya maafa katika ngazi za halmashauri. Sekretarieti za Mikoa zinapaswa kushirikisha Kamati za za Usimamizi wa Maafa ili kuimarisha uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau.

Post a Comment

0 Comments