Ticker

6/recent/ticker-posts

WAFANYABIASHARA TUNDURU WAHIMIZWA KUTOA RISITI STAHIKI ZA EFDKaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Bw. Joshua John akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi, mlango kwa mlango.

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Bw. Joshua John (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipofika wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango.

Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Godfrey Kumwembe akiwaelimisha wafanyabiashara na wauzaji wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.

Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Justine Katiti akimuelimisha mfanyabiashara wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. (PICHA ZOTE NA TRA).

**************************
Na mwandishi wetu
Tunduru

Wafanyabiashara wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wamehimizwa kutoa risiti stahiki kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi kudai na kukagua risiti kila wanaponunua bidhaa.

Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Joshua John wakati akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi, mlango kwa mlango.

“Natoa wito kwa wafanyabiashara wenye mashine za EFD kuhakikisha wanatoa risiti stahiki kila baada ya kufanya mauzo na wanunuzi wadai risiti na kuzikagua kama kiasi kilichoandikwa kinafanana na fedha waliyonunulia bidhaa, hii itasaidia kuongeza mapato ya serikali kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Bw. John.

Nae, Afisa Msimamizi wa Kodi wa TRA Mkoa wa Ruvuma Bw. Justine Katiti alielezea maendeleo ya kampeni hiyo tangu kuanza kwake tarehe 13 Oktoba, 2021, ambapo alisema kwamba, mpaka sasa maofisa hao wameshawafikia walipakodi takribani 1,000 katika wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa.

“Katika kampeni hii ambayo ilianza tarehe 13 Oktoba, 2021, tumefanikiwa kuwafikia wafanyabiashara wapatao 1,000 walioko katika Wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa. Kwa sasa tupo hapa wilayani Mbinga na tukimaliza tutaelekea Wilaya za Namtumbo na Madaba, alielezea Bw. Katiti.

Bw. Katiti aliongeza kuwa katika kampeni hiyo, pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara wamepewa elimu ya matumizi sahihi ya mashine za EFD.

“Tumefanikiwa kuwaelimisha masuala mbalimbali ya kodi ikiwepo matumizi sahihi ya mashine za EFD na kuwakumbusha kwamba, kutokutoa risiti ni kosa kwa mujibu wa sheria na adhabu yake ni kati ya Shilingi milioni 3 hadi 4.5 kwa mfanyabiashara atakayebainika hatoi risiti, aliongeza Bw. Katiti.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wa wilaya hiyo wamesema kuwa, wamefurahishwa na elimu iliyotolewa na maofisa hao wa TRA.

“Leo nimefurahi kutembelewa na maofisa wa TRA ambapo wamenifundisha kuwa makini na matapeli wanaojifanya watumishi wa TRA na wamenikumbusha kutoa risiti za EFD kila ninapofanya mauzo,” alisema Esau Pera ambaye ni mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo.

Rashid Mambulu ni mfanyabiashara wa vifaa vya umeme wilayani humo ambapo amewaomba wafanyabiashara wenzake kuzingatia utoaji wa risiti sahihi kwa wateja wao ili kuepukana na adhabu ya kutokutoa risiti za EFD.

“Kati ya mambo mengi niliyofundishwa na maafisa wetu wa TRA ni pamoja na kunikumbusha kukata risiti sahihi za EFD na wameniambia adhabu ya kutokutoa risiti ni shilingi milioni 3 hadi 4 na nusu hivyo nawaomba wafanyabiashara wenzangu tuzingatie utoaji wa risiti sahihi ili tuepukane na faini za kutokutoa risiti,” alieleza Bw. Mambulu.

Timu ya maofisa wanaofanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Ruvuma wako wilayani Tunduru wakiendelea kutoa elimu ya kodi na baada ya wilaya hiyo wataelekea Wilaya za Namtumbo na Madaba.

Post a Comment

0 Comments