Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI KATAMBI AWATAKA WAAJIRI KUWASILISHA MICHANGO WCF KABLA HAWAJASUKUMWA NA SHERIA

NA MWANDISHI WETU, MNAZI MMOJA, DAR


NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Patrobas Katambi, amewataka Waajiri nchini kuwasilisha michango kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa wakati kama ambavyo Sheria inavyowataka kufanya hivyo.

Katambi ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 14, 2021 alipotembelea banda la WCF kwenye Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Alisema Mfuko umekuwa ukifanya kazi nzuri sana katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo ni kulipa Fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.

“Na kwa ndugu zangu waajiri niwaombe sana jitahidini kupeleka michango kabla hamjasukumwa na sheria, jitahidini kuwasilisha michango kwa wakati ili iweze kuwafaa wafanyakazi wenu. “Alisisitiza Katambi.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma mpaka sasa Mfuko umeweza kusajili asilimia 90 ya waajiri wotenchini ambao wako kwenye kanzidata ya Mfuko

“Tunaendelea kuwahimiza Waajiri waendelee kuwasilisha michango yao kwa wakati na Mfuko uendelee kulipa Mafao kadri ya wale wanaohitaji wanavyojitokeza.” Alifafanua.

Alitoa wito kwa wadau wa Mfuko ambao ni Waajiri waendelee kushirikiana na Mfuko kama inavyopasa lakini pia wadau wengine ambao ni wale wanaopata Mafao, amewahakikishia kuwa Mfuko wao uko imara na unaendelea kutoa Mafao kwa Mujibu wa Sheria.

Akizunhumzia ushiriki wa Mfuko kwenye Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, Dkt. Mduma alisema “ Sekta ya Hifadhi ya Jamii ni moja ya Sekta pana ya Fedha na WCF ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wenye jukumu la kulipa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana kazi.

Alisema katika kufanya jukumu hilo Mfuko unashiriki katika shughuli za Uwekezaji kwa michango inayokusanywa inawekezwa kwenye maeneo mbalimbali.

“Utaona kwamba Mfuko unaingia kwenye sekta ya fedha katika Nyanja mbili ya kwanza kuratibu michango kama sekta ya hifadhi ya jamii lakini pia fedha zinazopatikana zinawekezwa na kwa kufanya hivyo tunashiriki katika sekta pana ya fedha.” Alisema Dkt. Mduma.

Kwa mujibu wa waandaaji wa maadhimisho hayo, Wizara ya Fedha na Mipango, walengwa wakuu wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo: watumishi wa umma; wanafunzi; wakufunzi; wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu; wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs); asasi za kiraia; Wahariri na waandishi wa vyombo vya habari; watoa huduma za fedha; na umma kwa ujumla.

Lengo la Maadhimisho hayo yaliyoanza Novemba 8 na yanatarajiwa kufikia kilele Novemba 14, 2021 ni kuhakikisha Umma wa Watanzania unaelewa vema fursa zilizopo kwenye sekta ya fedha, ili kuinua vipato vyao na hatimaye kukuza uchumi wa taifa.


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. John Mduma (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Mfuko, Bi. Laura Kunenge, akizunguzma kwenye banda la WCF kwenye Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Novemba 14, 2021.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi
Mhe. Katambi akisaini kitabu cha wageni.
Mhe. Katambi akipokea zawadi ya kifuniko cha gurudumu la gari (Wheel cover) na mfuko wenye vipeperushi na taarifa zihusuzo Mfuko.
Afisa wa WCF, Bi. Janeth Ishengoma, akimsikiliza Mwananchi aliyefika kupata elimu kwenye banda la WCF.

Afisa Mwandamizi Uwekezaji WCF, Bw.Michael Semiono (wakwanza kushoto) na Bi. Jannet Ishengoma wakitoa elimu kwa wananchi kwenye banda la Mfuko.

Post a Comment

0 Comments