Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI MOLLEL :'WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA WASAIDIWE KIUCHUMI'


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akizungumza leo November 20,2021 Jijini Tanga wakati akihikitimisha shughuli za Kampeni Maalum ya Kujenga uelewa kwenye Jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya iliyofadhiliwa na Shirika la Cassa Familia Rosetta pamoja na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimisha shughuli za Kampeni Maalum ya Kujenga uelewa kwenye Jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya iliyofadhiliwa na Shirika la Cassa Familia Rosetta pamoja na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) leo November 20,2021 Jijini Tanga

..................................................................

Na WAMJW – Tanga.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo nchini kuwasaidia waraibu waliotoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kuanzisha shughuli za kiuchumi na kuepuka kurudi katika matumizi ya dawa za kulevya.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Tanga akihikitimisha shughuli za Kampeni Maalum ya Kujenga uelewa kwenye Jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya katika Jiji hilo pamoja na Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga iliyofadhiliwa na Shirika la Cassa Familia Rosetta pamoja na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

“Halmshauri pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya nawaomba katika mipango ya kuwasaidia wanawake na vijana katika ile asilimia 10 ya mapato yenu basi msiwaache hawa ambao wametoka kwenye uraibu wa madawa tuwape nao kipaumbele ili wasirudi katika matumizi ya dawa hizo” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amesema kuwa Mkoa wa Tanga ni wa Pili kwa kuwa na idadi kubwa ya waraibu wa madawa ya kulevya huku takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Mkoa huo kuwa na zaidi ya waathirika 5190 huku Mkoa wa Dar Es Salaam ukiongoza kuwa na warahibu wengi wa dawa za kulevya.

“Kampeni hii ya kujenga uelewa na uanzishwaji wa huduma za matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya zimefika kwa wakati muafaka ili kuweza kusaidia kuvunja mnyororo wa changamoto za utumiaji wa mihadarati na madawa ya kulevya” amesema Dkt. Mollel.

Kampeni hiyo iliyoanza Mwezi Mei, 2021 na kuhitimishwa Oktoba 2021 imeweza kuwafikia waraibu 879 ambao katik yao 63 wameweza kuanzishiwa dozi ya Methadone katika Kliniki iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bombo huku waraibu wengine wakiendelea kuongezeka kutaka kuanza kutapa huduma ya methadone.

Aidha Dkt. Mollel amewashukuru waratibu wa kampeni hiyo pamoja na Walimu wa Shule Msingi na Sekondari walioshiriki katika kutoa elimu ya athari za dawa za kulevya kwa zaidi ya wanafunzi 7000 katika Wilaya ya Muheza pamoja na wanafunzi zaidi 20,000 katika Jiji la Tanga.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Thobias Mwilapwa amesema kuwa kupitia kamati ya Ulinzi na Usalama anayoisimamia katika Wilaya hiyo, wastani wa watu 6 hukamatwa kila siku kwa makosa ya matumizi na kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi au herion.

“Bado Tanga inaonekana ni lango la kuingia kwa dawa za kulevya nchini, nimeshatoa maelekezo kwa kamati ya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika kudhibiti mianya ya uingiaji na matumizi ya dawa za kulevya katika Wilaya ya Tanga na tutaendelea kudhibiti matukio yanayohamasisha matumizi ya dawa za kulevya” amesema Mhe. Mwilapwa.

Post a Comment

0 Comments