Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATAKA WANUFAIKA WA MAFUNZO YA JICA KUWAPATIA WAMACHINGA TAA ZINAZOTUMIA NISHATI YA JUA


Wanachama wa JATA wakiwa wameshika taa za kukodi zinazotolewa na WASSHA Inc wakati wa ziara ya kikazi katika kijiji cha Mindu WASSHA Kiosk katika kijiji cha Mindu, mkoani Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando akizungumza na wafanyakazi wa JATA na WASSHA wakati wa semina ya siku moja iliyofanyika katika eneo la WASSHA (muuzaji wa taa za nishati ya jua) mkoani Morogoro.

*********************************

Morogoro. Serikali imewataka wanachama wa Chama cha Wanafunzi waliosoma Japan au nchi nyingine chini ya ufadhili wa JICA (JATA) kuongeza uelewa na kuwasambazia wafanyabiashara wadogo, maarufu kama "Wamachinga", taa bora na za bei nafuu zinazotumia nishati ya jua katika maeneo yao ya biashara ili kuongeza muda wa kufanya kazi zao.

Akizungumza katika semina ya siku moja na WASSHA Inc, kampuni ya Kijapani inayotoa huduma ya kukodisha vifaa vya umeme wa jua kwa bei nafuu katika maeneo yasiyo na umeme wa gridi ya taifa kupitia vioski (maduka ya rejareja), Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando alisema maeneo mengi ya soko ambapo wafanyabiashara wadogo walihamishiwa bado hawana miundombinu mizuri ya umeme, hali inayopelekea kupata ugumu wa kufanya kazi wakati wa usiku.

"Kwa sasa bado ni vigumu kwa Machinga wetu kufanya biashara zao wakati wa usiku katika maeneo yao ya sasa. Nawaomba wanachama wa JATA kupitia kampuni ya WASSHA kuwakodishia taa za umeme wa jua kwa bei rahisi ambayo wataweza kuimudu ili kuongeza muda wao wa kufanya kazi wakati wa usiku," alisema.

Katika hatua nyingine, Msando alitoa shukrani zake kwa JATA kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo, ambayo inanufaisha wakazi wa kipato cha chini wakiwemo wajasiriamali wadogowadogo.

Alisema uanzishwaji wa miradi hiyo unaendana na mipango ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Wanachama wa JATA ni maafisa mbalimbali kutoka taasisi za umma na binafsi ambao walisoma au kuhudhuria programu za mafunzo na semina nchini Japan kama sehemu ya ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na serikali ya Japan kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA).

Mwenyekiti wa Taifa wa JATA, Gregory Mlay alisema chama kinatekeleza miradi sita katika sekta mbalimbali kila mwaka ndani ya mikoa tofautitofauti chini ya msaada wa karibu wa JICA.

Mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Dk Severine Assenga alisema JATA ina wanachama zaidi ya 4,000 nchi nzima ambao kwa namna moja au nyingine walisomea Japan na chi zingine chini ya ufadhili wa JICA.

Wanachama hao walifanya ziara katika eneo la biashara la kampuni ya WASSHA na kufanya semina mnamo Oktoba 30, 2021 kujifunza jinsi nishati safi ya jua inavyohudumia watu wa kipato cha chini kama huduma na biashara.

Semina hiyo iliandaliwa ili kuelewa mtindo wa biashara wa WASSHA na faida zake kwa maendeleo ya maisha ya watu nchini Tanzania.

WASSHA imekuwa ikitoa huduma ya umeme wa jua katika mikoa ya Tanzania kama vile Dar es Salaam, Pwani na Morogoro n.k chini ya msaada wa karibu kutoka JICA tangu mwaka 2016. Ilikuwa mradi wa kwanza waMfuko wa Fedha za Uwekezaji wa Sekta Binafsi (PSIF) za JICA katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Wanachama wa JATA pia walitembelea mawakala na watumiaji wa taa za WASSHA waliopo Manispaa ya Morogoro na kando ya barabara ya Kigurunyembe – Mkuyuni kushuhudia na kuzungumza na wanufaika wa mradi huo.

Wanachama waliona na kuelewa mfano wa biashara, faida za huduma za WASSHA kwa jamii na jinsi kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli zake kupitia ujumbe wake wa "nguvu kwa watu".

Post a Comment

0 Comments