





*******************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Wadau wa maendeleo nchini wameombwa kujitokeza kuunga mkono juhudi za maendeleo ya jamii kwa kuleta suluhu za matatizo yanayoikabili ikiwemo kutoa mafunzo ya afya, maadili na elimu kwa watoto na vijana.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Community Hands Foundation, Bw.Paul Makoe wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Elimika uliozinduliwa leo katika shule ya msingi ya Mchikichini iliyoko Mbagala Zakhem, Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam yenye lengo la kuwafundisha watoto na vijana kuhusu afya, maadili na Malezi.
Amesema kuwa lengo la uzinduzi wa Mradi huo ni kutokana na tafiti ndogo waliyofanya na kukutana na malalamiko kutoka kwa Walimu na walezi ya uwepo wa upotovu wa maadili kwa wanafunzi hivyo kuja na mpango wa utoaji wa elimu hiyo.
"Mradi huu ni wa miaka mitano na tunatarajia kufikia zaidi ya Mikoa 20 ya Tanzania hivyo tunaomba wadau na taasisi nyingine kujitokeza kuunga mkono juhudi hizi tunazozitoa kuhakikisha jamii inapata uelewa kamili". Amesema Bw.Makoe.
Aidha amesema kuwa kama wanafunzi na vijana wakipatiwa elimu hiyo na kuitatua itawasaidia kukabiliana na magonjwa na maisha ya kila siku yanayozunguka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shule ya Mchikichini Bw.Bonifance Njavike amesema kuwa ujio wa taasisi hiyo utaleta manufaa hivyo itasaidia watoto katika makuzi yao hasa ya kimaadili.
Naye Mjumbe wa kamati ya shule ya Mchikichini Bi.Elizabeth George amesema kuwa utolewaji wa elimu hiyo imekuja muda muafaka hivyo itasaidia Watoto kutokuwa na malezi mabaya.
Awali akizungumza Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mchikichini Mwl.Erenest Kibwinya ameishukuru Taasisi hiyo kwa hatua ya utolewaji wa elimu hiyo na kuomba taasisi zingine kuiga mfano huo.
0 Comments