Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akizungumza na ujumbe wa Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Posta Burundi wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Posta Burundi Bi. Lea Ngabire walipotembelea Mamlaka hiyo kwa ziara ya mafunzo. Picha na: TCRA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Posta Burundi Bi. Lea Ngabire akisaini Kitabu cha Wageni wakati alipotembelea Makumbusho ya Mawasiliano iliyopo Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Katika ziara hiyo ya mafunzo Ingabire aliambatana na Maafisa Waandamizi wa Posta Burundi. Picha na: TCRA
**************************
Na: Mwandishi wetu
Shirika la Posta la nchini Burundi limeweka bayana dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya Posta nchini humo ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi zaidi katika usimamizi wa masuala ya Posta.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya posta wa Burundi Bi. Lea Ngabire wakati alipozuru Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania akiambatana na ujumbe wa Maafisa waandamizi wa Posta Burundi katika ziara ya mafunzo.
“Tumefika hapa TCRA na kujionea shughuli mbalimbali za mawasiliano na lengo letu ni kuona namna nchi zetu mbili zinavyoweza kushirikiana katika kukuza na kuendeleza sekta ya posta” alibainisha Ngabire.
Ujumbe wa Maafisa hao umejumuisha Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Posta Burundi Nyayishimiye Olivier na Mkuu wa masuala ya Barua Misirakuba Deo.
Akipokea ujumbe huo mnamo Jumatano Tarehe 17 Novemba 2021 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari aliwakaribisha na kuwaeleza kuwa TCRA kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano nchini Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa mawasiliano hasa kikanda na imekuwa mshirika muhimu wa mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inasimamiwa kwa uthabiti na kwa upande wa posta TCRA imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa na kama mnavyofahamu pia Makao Makuu ya Posta Afrika yapo hapa nchini” alibainisha na kuongeza Jabiri.
Pembezoni mwa mazungumzo na ujumbe huo pia, Mkurugenzi Mkuu Jabiri aliwaeleza wajumbe hao kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano barani Afrika inaimarika na ndiyo sababu imekuwa ikishirikiana na Shirika la Posta Afrika (PAPU) kuhakikisha ujenzi wa Ofisi ya PAPU makao makuu ambayo ujenzi wake unaendelea jijini Arusha unakamilika kwa wakati ambapo matarajio ni kukamilisha ujenzi wa jingo la kisasa jijini Arusha itakapowadia 2022.
Nae Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA Dkt. Emmanuel Manasseh ambae sekta ya Posta inasimamiwa na kurugenzi anayoingoza alibainisha kwamba hakuna namna uchumi wa kisasa utajengwa bila kuhusisha posta kwani sekta hiyo ni muhimu katika masuala ya usafirishaji na ufikishaji wa taarifa mbalimbali zinazowezesha kujenga uchumi wa kisasa (Uchumi wa kidijitali).
“Tunapoenda kwenye uchumi wa kidijitali posta ni sekta muhimu sana ambayo hatuwezi kukwepa kuitumia kwani itatuwezesha kufikia azma ya kujenga uchumi wa kidijitali.” Alisisitiza Dkt Manasseh.
Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo ujumbe huo ulibainisha kufurahishwa na maarifa waliyopata baada ya kutembelea TCRA ili kujifunza na kuahidi kwamba watatendea kazi yale waliyojifunza katika kukuza sekta ya Posta nchini Burundi.
0 Comments