Ticker

6/recent/ticker-posts

TIA YAVUNA MAELFU YA WAHITIMU KAMPASI ZA SINGIDA, MWANZA NA KIGOMA


Mgeni rasmi wa Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu wa pili kushoto, akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Dk. Momole Kasambala (wa kwanza kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakili Said Chiguma muda mfupi kabla ya kuanza kwa mahafali hayo yaliyojumuisha Kampasi za Taasisi hiyo kwenye mikoa ya Singida, Mwanza na Kigoma mkoani Singida jana.


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu (katikati) aliyemwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Nchemba, akifuatilia matukio mbalimbali wakati wa mahafali hayo.
Wahitimu wa fani mbalimbali wakiwa kwenye sherehe za mahafali hayo.

Baadhi ya wahitimu wakijiandaa kutunukiwa.

Sherehe zikiendeleaSherehe zikiendelea


Wahitimu wakiwa kwenye sherehe.

*****************************

Na Mwandishi Wetu, Singida

TAASISI ya Uhasibu nchini (TIA) kupitia Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma imefanya maboresho makubwa ya kidijitali kwenye mifumo ya utoaji mafunzo, sambamba na miundombinu ya kujifunzia, huku muda wowote kuanzia sasa ikitarajia kuanza kuendesha baadhi ya Programu zake kwa njia za Mtandao (e-Learning).

Akizungumza kwenye Mahafali ya 19 iliyojumuisha Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma mkoani hapa jana, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Dk. Momole Kasambala, alisema kwa sasa Taasisi hiyo imeendelea kuboresha njia za ufundishaji ikiwa ni pamoja na kuingiza mitaala ya ‘TEHAMA’ katika ngazi zote.

“Tunaishukuru Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa kazi nzuri na ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika kumshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango juu ya masuala mbalimbali ya Taasisi ili kuendana na mahitaji ya soko sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia” alisema Kasambala.

Jumla ya wahitimu 3,116 walitunukiwa Cheti cha Awali, Astashahada, Stashahada, na Shahada katika fani mbalimbali kwa kampasi za mikoa ya Singida, Mwanza na Kigoma, huku idadi ya wahitimu wote wa TIA kwa mwaka wa masomo 2020/2021 katika kampasi za Dar es Salaam, Mbeya, Singida, Mtwara, Mwanza na Kigoma ikifikia 12,278.

Kasambala alibainisha kuwa mvuto wa ongezeko hilo kwa kiasi kikubwa linatokana na ubora wa elimu itolewayo unaotokana na mitaala inayowajengea wanachuo wa ngazi zote msingi wa umahiri ( competency), hivyo kumwezesha mhitimu kuajiriwa na hata kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake.

Aidha, alisema utaratibu mzuri wa serikali wa kuwapangia vyuo moja kwa moja wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo. Mathalani, katika mwaka wa masomo 2021/2022 jumla ya wanafunzi 2,560 kutoka maeneo mbalimbali nchini, wamepangwa kujiunga na kozi mbalimbali za cheti cha awali katika kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma.

Pia suala lingine lililochagiza ni ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada hatua ambayo imewezesha watanzania wengi wenye sifa kumudu gharama za masomo. Ambapo kwa 2021/2022 serikali imepanga kuwafadhili wanachuo 401 wa shahada katika Kampasi ya Singida ikiwa ni ongezeko la asilimia 39.4 na wanachuo 180 wa kampasi ya Mwanza sawa na ongezeko la asilimia 38.3.

Kwa upande wa miundombinu ya kusomea na kufundishia, TIA imeendelea kuboresha na kuongeza miundombinu ili kuhakikisha ongezeko la wanachuo linakwenda sambamba na ubora na idadi ya miundombinu,” alisema Afisa huyo Mtendaji Mkuu.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Khatib Kazungu kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba, alipongeza TIA kwa jitihada mbalimbali za maboresho huku akishauri taasisi hiyo kuendelea kubuni mbinu zaidi za kujiimarisha katika utoaji wa huduma za utafiti na ushauri.

“Pia nawapongeza kwa jitihada zinazoendelea katika kampasi za Mwanza na Kigoma, kuhakikisha mnahamia katika majengo yenu mapema iwezekanavyo, lakini nimefurahishwa na jitihada pamoja na mchango wa Taasisi hii kwa taifa letu upande wa kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali pamoja na wajasiriamali wadogo. ” alisema Kazungu.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakili Said Chiguma aliwaasa wahitimu wote kuitafakari na kuiishi dhana ya elimu waliyopatiwa kwa kuzingatia nukuu za Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema “Elimu ni mchakato unaomwandaa mtu aweze kukabiliana na mazingira anayoishi” “Elimu ni silaha, ni kifaa kilicho kimya lakini chenye matokeo makubwa kwa Taifa.”

Pamoja na mambo mengine, majukumu makuu ya TIA ni kutoa Mafunzo, kufanya Utafiti na kutoa Huduma ya Ushauri kwenye fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma, Uhasibu wa Umma na Fedha, Usimamizi wa Miradi na katika nyanja nyingine za kibiashara.

Post a Comment

0 Comments