Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA BALOZI WA ANGOLA NCHINI


Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba (kulia) akizungumza na Balozi wa Angola Mhe. Sandro Renato Agostinho De Oliveira katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati tarehe 25 Novemba, 2021 jijini Dar-es-salaam.


Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akizungumza na Balozi wa Angola Mhe. Sandro Renato Agostinho De Oliveira (Hayumo pichani) katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati tarehe 25 Novemba, 2021 jijini Dar-es-salaam.


Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Angola Mhe. Sandro Renato Agostinho De Oliveira katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati tarehe 25 Novemba, 2021 jijini Dar-es-salaam mara baada ya kumaliza mazungumzo.

**********************

Waziri wa Nishati Mhe. January Yusuf Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Angola nchini Tanzania Mhe. Sandro Renato Agostinho De Oliveira kwa lengo la kujadili maeneo ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola katika sekta ya nishati.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 25 Novemba, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar-es-salaam wakiwemo wawakilishi kutoka pande zote mbili za Tanzania na Angola.

Kupitia kikao hicho, Waziri Makamba na Balozi Sandro Renato Agostinho De Oliveira walijadili maeneo kadhaa ya ushirikiano katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

Maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala ya biashara ya gesi iliyosindikwa (Liquefied Natural Gas - LNG); programu za kujengeana uwezo kama vile mafunzo, warsha na makongamano; uanzishwaji na uendeshaji wa hifadhi za kimkakati za bidhaa za petroli (strategic petroleum reserves) na biashara ya mafuta.

Maeneo mengine ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za fursa zilizopo katika biashara ya gesi ya kwenye mitungi (Liquefied Petroleum Gas), viwanda vya petrokemikali; mitambo ya kusafisha mafuta ghafi (refineries) na kubadilishana data na taarifa za kitaalamu zinazohusiana na sekta ya mafuta na gesi asilia.

Katika kuhitimisha, Waziri Makamba alieleza kuwa Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Angola hususan katika masuala ya mafuta kwani nchi hiyo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika.

Kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2020 Angola ilishika nafasi ya pili kwa uzalishalishaji wa mafuta barani Afrika ikitanguliwa na Nigeria.

Naye Balozi wa Angola nchini alieleza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Angola utazinufaisha sana nchini hizi na kwamba Angola inaendela kujifunza kutoka Tanzania kuhusu miradi mikubwa ya kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwemo mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima – Uganda hadi Chongoleani Tanga – Tanzania na miradi ya usambazaji gesi asilia inayotekelezwa nchini.

Tayari Tanzania na Angola zimeanza mchakato wa kuwa na Mkataba wa Makubaliano ya Awali (Memorundum of Understanding – MoU) itakayoongoza ushirikiano wa nchi hizi katika sekta za madini, mafuta na gesi asilia tangu mwaka 2019.

Post a Comment

0 Comments