Ticker

6/recent/ticker-posts

ZIMAMOTO YAPATA UGENI KUTOKA HAMBURG, UJERUMANI


Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga (Kushoto), Akizungumza na Ndugu Reinhard Paulsen (Katikati) kutoka Jiji la Hamburg Nchini Ujerumani alipomtembelea ofisini kwake leo tarehe 25 Novemba, 2021 Jijini Dodoma.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga (Kushoto), akikabidhi zawadi ya kikombe chenye maneno “Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na namba ya Dharura 114” kwa mgeni wake ndugu Reinhard Paulsen (Kulia) kutoka Jiji la Hamburg Nchini Ujerumani leo tarehe 25 Novemba, 2021 Makao Makuu ya Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma. 


Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga (Katikati) akiongoza kikao na wageni kutoka Jiji la Hamburg Nchini Ujerumani walipomtembelea ofisini kwake leo tarehe 25 Novemba, 2021 Jijini Dodoma; Kikao ambacho kilihudhuriwa pia na Viongozi Waandamizi wa Jeshi hilo. 


Picha ya pamoja ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga, Viongozi Waandamizi wa Zimamoto Na Uokoaji pamoja na wageni kutoka Jiji la Hamburg Nchini Ujerumani katika Ofisi za Makao Makuu ya Zimamoto Na Uokoaji Jijini Dodoma leo tarehe 25 Novemba, 2021. (Picha zote na Jeshi la Zimamoto Na Uokoaji) 

******************** 

Dodoma, 25 Novemba 2021. 

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga, leo tarehe 25 Novemba, 2021 amepokea Wataalamu wa Uzimaji Moto na Maokozi kutoka Jijini Hamburg, Ujerumani na kufanya nao kikao kifupi akiwa pamoja na Viongozi Waandamizi wa Jeshi hilo. 

Kamishna Jenerali amepokea ugeni huo akiwa ofisini kwake Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma. Ugeni huo uliongozwa na Ndugu Reinhard Paulsen akiongozana na Nobert Sorge pamoja na Dennis Rosenthal hao ambao ni wazimamoto wa kujitolea chini ya program ya ‘’sistership cities’’ na kuwashukuru sana kwa misaada mbalimbali ya vifaa pamoja na mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa nchini Ujerumani. 

“Baadhi ya maafisa na askari wamefaidika sana na mafunzo ya maokozi pamoja na huduma ya kwanza, lakini pia imekuwa ni fursa kwa Jeshi kupokea wakufunzi mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa mafunzo hapa nchini” alisema Kamishna Jenerali Masunga. Aliendelea kusema kwamba bado Jeshi linahitaji msaada mkubwa sana katika mafunzo ya maokozi angani ‘’High Angel Rescue’’, mafunzo ya utoaji huduma ya kwanza pamoja na misaada ya vifaa vya maokozi na uzimaji moto. 

Naye kiongozi wa ugeni huo, Ndugu Reinhard Paulsen, alimshukuru sana Kamishna Jenerali na kusema; “Tunashukuru sana kwa mapokezi mazuri lakini pia kwa namna ambavyo Jeshi limepiga hatua kubwa ya mabadiliko chanya kwa kipindi kifupi na kutunza vifaa mbalimbali ambavyo vimekuwa vikiletwa kutoka nchini Ujerumani”. 

Paulsen alisema kupitia mpango wa Sistership Cities tuko tayari kuendelea kutoa misaada ya vifaa pamoja na mafunzo kwa maafisa na askari. Aidha kwa sasa tunaendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huu wa Uviko ambao ni janga la kidunia na tunaahidi kushirikiana kwa kadiri itakavyowezekana. 

Kamishna Jenerali alihitimisha ziara ya ugeni huo kwa kufanya kikao kifupi na baadhi ya Viongozi Waandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wageni hao.

Post a Comment

0 Comments