Ticker

6/recent/ticker-posts

KIJUKUU CHA BIBI K: WAFANYABIASHARA MSIPUUZE REDIO ZA KIJAMII

Meneja Vipindi na Uzalishaji wa Kahama Redio William Bundala akitoa Somo la umuhimu wa Redio za kijamii katika kukuza biashara.
Mgeni Rasmi aliyefunga kongamano hilo Mhe. Injinia Stella Manyanya akimkabidhi cheti Cha uwezeshaji Kijukuu cha Bibi K


Washiriki wa mafunzo wakimsikiliza kwa makini Kijukuu cha Bibi K hayupo pichani


**********************

Na Mwandishi wetu- Dodoma


Wafanyabiashara na wananchi wametakiwa kuziamini na kuzitumia Radio za kijamii zilizopo nchini ili kutangaza biashara zao na kupata habari za uhakika kwani ndiyo redio pekee zizowafika wananchi kwa haraka na uhakika zaidi.


Wito huo umetolewa leo Jijini Dodoma na Meneja wa Vipindi na Uzalishaji wa Kahama Redio William Bundala (Kijukuu cha bibi K) wakati akiwasilisha somo la umuhimu wa Redio za Kijamii,Mafanikio na changamoto katika Toleo la pili la warsha ya wadau wa Shule ya usimamizi wa mtandao Jamii Tanzania.


Bundala amesema kuwa Wafanyabiashara wengi hawaziamini Redio za kijamii katika kutangaza biashara zao kwa imani kuwa redio hizo hazifiki umbali mrefu na hazina wasilikilizaji wengi.


Akitolea ufafanuzi Bundala amesema kuwa ni kweli redio za kijamii hazisikiki umbali mrefu ila maeneo ambayo zipo zinasikika kwa kiwango kikubwa na kwamba unapotangaza na redio za kijamii una uhakika wa kumfikia mteja kwa asilimia 100% pale biashara yako ilipo.


Sambamba na hayo Bundala ameongeza kuwa redio za kijamii zina uhakika wa kuwafikia wasikiliza wa eneo husika na kwamba hata redio na Televisheni kubwa zenye leseni ya kitaifa zinatumia redio za kijamii wanapokuwa na shughuli za Matamasha katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini.


Kuhusu wananchi kuwa na imani na Taarifa za habari za vyombo vyenye leseni kubwa Bundala amesema kuwa redio zote vyanzo vyake vinafanana isipokuwa redio za kijamii zinachofanya ni ujanibishaji (localization) wa habari hizo ili zisadifu uhalisia wa mazingira ya jamii wanazozihudumia.


Nao baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo wamezipongeza redio za kijamii nchini kwa kazi kubwa wanazofanya ikiwa ni kuibua changamoto mbalimbali za kijamii pamoja na kuweka maudhui tofauti tofauti katika vipindi vyao.


Toleo la pili la warsha ya wadau wa Shule ya usimamizi wa mtandao Jamii Tanzania lililofanyika Dodoma limeshirikisha wadau 80 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania,Kenya,Uganda,Zimbabwe,Afrika Kusini,India,Uingereza,Mauritius,Norway na Marekani.


Toleo hili la mwaka 2021 limeandaliwa na Tanzania Community Networks Alliance, Kondoa Community Network Cooperative Society Ltd, Kasulu Community Network Cooperative Society Ltd na Nyasa Community Network Cooperative Society Ltd na Limedhaminiwa na Internet Society, Association of Progressive Communications, Alliance for Affordable Internet, AFRINIC, TechSonic na Basic Internet Foundation.

Post a Comment

0 Comments