Ticker

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA: TANZANIA IKO MIKONONI MWA MUNGU


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua msikiti wa Nkowe wilayani Ruangwa, baada ya kushiriki sala ya Ijumaa, Septemba 31, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Msikiti wa Nkowe wilayani Ruangwa baada ya kushiriki sala ya Ijumaa katika Msikiti huo, Desemba 31, 2021. Kushoto Shekh wa wilaya hiyo, Hashim Lyambamba na kulia ni Katibu wa BAKWATA Wilaya, Mohammed Juma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

***********************************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko mikononi mwa Mungu na ndiyo maana imeendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu na kimbilio la mataifa yaliyopoteza tumaini.

“Nchi hii imeshikwa na Mwenyezi Mungu na ni kwa sababu viongozi wa dini wanaendelea kuliombea Taifa hili, kwa hiyo na sisi tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba nchi hii inabaki kwa salama,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Desemba 31, 2021) wakati akizungumza na waumini baada ya kushiriki ibada ya Ijumaa na kuzindua msikiti wa Nkowe, ulioko kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Amesema Serikali zote tangu awamu ya kwanza hadi ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, zimeendeela kuheshimu uwepo wa dini nchini kwani miongozo na mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini mbalimbali yanawafanya waumini wao kuwa rai wema.

“Mheshimiwa Rais alipoingia madarakani alikutana na Mababa Askofu wote wa nchi hii, lakini pia alikutana na masheikh wote kupitia BAKWATA ili kupata miongozo na baraka za kuongoza nchi hii.”

Waziri Mkuu amewataka Watanzania wampe nafasi Rais Samia ya kufanya kazi kwa sababu amekuwa Serikalini kwa muda mrefu na anajua ni nini Watanzania wanatamani Serikali yao iwafanyie.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema madaraka yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na yeye ndiye hupanga nani awe nani na kwa wakati gani. “Tuache tabia ya kuwafanya viongozi washindwe kufanya kazi zao kwa kuwatengenezea migogoro ya kila siku, tena mengine ya kusingizia tu.”

“Kila nafasi imetengenezwa na Mwenyezi Mungu na kila anayekwenda kuongoza Mwenyezi ndiye amesema wewe utakuwa pale. Na kama hajasema, hutokuwa; utatumia hela nyingi na zitapotea bure. Utakwenda na mambo mengine ya giza, lakini hutomudu. Mwenyezi Mungu keshasema huyu ni huyu, tuwaheshimu walioko kwenye nafasi za kuwatumikia Watanzania wafanye kazi zao kwa weledi.”

Akizungumzia juhudi zinazofanywa na Serikali, Waziri Mkuu amesema hivi karibuni Serikali imetoa sh. bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vituo vya afya wilayani Ruangwa. Amesema wilaya hiyo ina uhakika wa kuwapeleka shule kwa wakati watoto wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kwani madarasa yapo ya kutosha.

Waziri Mkuu yuko jimboni kwake Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Post a Comment

0 Comments