Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO AAGIZA KUSIMAMISHWA KWA MKATABA BAINA YA JIJI LA DODOMA NA KAMPUNI YA GREEN WASTE


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akishuhudia takataka zilizoachwa kandokando ya barabara zaidi ya wiki mbili baada ya kukusanywa katika maeneo ya Majengo Jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kustukiza katika maeneo hayo. Januari 15,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru (mwenye suti ya kijivu) juu ya kufanya zoezi la usafi kuwa endelevu katika jiji hilo wakati alipofanya ziara katika soko la Majengo. Januari 15,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe wakati alipofanya ziara katika soko la Majengo kukagua zoezi la usafi katika eneo hilo. Januari 15,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitembelea soko la Majengo lililopo Dodoma kukagua utekelezaji wa zoezi la usafi katika soko hilo. Januari 15,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na wafanyabiashara wa soko la majengo kuwaagiza kufanya zoezi la usafi kuwa endelevu katika maeneo yao wakati alipotembelea soko hilo tarehe 15 Januari 2022.


PICHA – OFISI YA MAKAMU WA RAIS

**********************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 15 Januri 2022 ametembelea katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dodoma pamoja na Soko la Majengo kukagua utunzaji wa Mazingira katika maeneo hayo.

Akiwa katika mitaa hiyo Makamu wa Rais ameshuhudia uwepo wa takataka katika maeneo mbalimbali ambazo wananchi wamezikusanya lakini huchukua muda mrefu pasipo kuondolewa.

Wananchi hao wamemueleza Makamu wa Rais adha wanayoipata ya kuishi na takataka hizo jirani na maeneo yao kwa kipindi cha wiki mbili pasipo kuondolewa hali inayohatarisha usalama wa afya zao. Aidha wamesema licha ya kutoa fedha kwa mamlaka zinazokusanya takataka hizo lakini bado takataka hizo husalia katika maeneo yao ambayo pia hutumika kwa biashara za vyakula.

Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea maeneo hayo, Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na hali ya usafi katika mkoa wa Dodoma. Ameagiza kusimamishwa kwa mkataba baina ya Jiji la Dodoma na kampuni inayokusanya taka hizo (Green Waste) kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake kiufanisi.

Amewataka viongozi wa Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka katika kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi pamoja na maeneo ya masoko na barabara zote. Aidha Makamu wa Rais amewaagiza wakurugenzi katika maeneo mengine nchi nzima kuchukua zoezi la usafi kama zoezi endelevu na linapaswa kuzingatiwa kikamilifu. Amewataka viongozi kuacha kukaa ofisini pekee bali pia kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yao ili kufuatilia wale waliowapa dhamana ya uondoaji wa takataka hizo katika mitaa kama wanakidhi kuendelea kufanya kazi hiyo.

Post a Comment

0 Comments