Ticker

6/recent/ticker-posts

MRITHI WA MAALIM SEIF KUPATIKANA JANUARI 29************

NA JUMA ISSIHAKA


CHAMA cha ACT Wazalendo, kinatarajia kumpata mrithi wa nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu Mwenyekiti na Mjumbe wa Halmashauri Kuu taifa ya chama hicho, Januari 29, mwaka huu.


Hatua hiyo inatarajiwa kufikiwa wakati wa Mkutano Mkuu Maalum utakaofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.


Akizungumzia mkutano huo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Saibu, alisema pamoja na ajenda ya kujaza nafasi ya Mwenyekiti, Makamu wake na Mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu, pia mambo mbalimbali yatafanyika.


Aliyataja mambo hayo ni uzinduzi wa programu tumizi ya ACT Kiganjani itakayofanya mageuzi ya uendeshaji wa chama hicho kwenda kisasa na uzinduzi wa utaratibu wa kuisimamia na kuiwajibisha serikali nje ya bunge.


“Mkutano wetu kwa mujibu wa Katiba utatanguliwa na matukio kadhaa tutaanza na kikao cha Kamati Kuu ya Chama kitakachofanyika Januari 27, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City,” alisema.


Mbali na Kamati kuu, alibainisha mkutano huo utatanguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa itakayoketi Januari 28, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City.


Alieleza pia watafanya mdahalo utakaotoa nafasi kwa wagombea wa nafasi zilizowazi ndani ya chama hicho, kujinadi mbele ya viongozi wa ACT Januari 28, mwaka huu.


Aidha, alisema katika mkutano huo, viongozi wa vyama mbalimbali nje ya nchi na rafiki wa ACT Wazalendo vimealikwa kushiriki.


Alivitaja vyama hivyo na nchi zao katika mabano ni NDC Alliance (Zimbabwe), ODM (Kenya), NUP (Uganda), UPND (Zambia), UTM (Malawi) na UNC (Congo).


Mbali na viongozi wa vyama hivyo kushiriki mkutano huo, Shaibu alisema wageni wengine kutoka ndani ya nchi watahudhuria wakiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, wanazuoni, wanaharakati na wasanii watatumbuiza.


Alimtaja mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa kiongozi wa chama cha NDC Alliance cha Zimbabwe, Nelson Chamisa.


Kuhusu ushiriki wa vyama vingine vya siasa nchini katika mkutano huo, Shaibu alifafanua kwamba vyote vimealikwa na anatarajia vitahudhuria.


ACT Wazalendo kinajaza nafasi ya Mwenyekiti wake, baada ya aliyekuwa na wadhifa huo, Maalim Seif Sharif Hamad, kufariki dunia Februari 17, mwaka jana.


Wagombea waliochukua fomu kuwania nafasi ya Mwenyekiti ni Juma Duni Haji na Hamad Masoud Hamad.


Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar inawaniwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman na Juma Said Sanani.


Kwa upande wa wagombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Tanzania bara ni Chrisant Msipi, Ester Thomas, Fungo Godlove, Johnson Mauma, Msafiri Mtemelwa, Jafet Masawe na Fidel Hemed.

Post a Comment

0 Comments