Ticker

6/recent/ticker-posts

MSAJILI MABARAZA AJA NA MIKAKATI YA KUPUNGUZA MASHAURI YA ARDHI NCHINI

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Profesa Ibrahim Juma akisoma kipeperushi katika Banda la Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2022.

Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Stella Tullo (Kushoto) akimfafanua jambo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya Dodoma Jackson Kanyerinyeri (Kushoto) akimsikiliza mwananchi aliyefika Banda la Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya katika maonesho ya wiki ya sheria yanayoendelea jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sajini akitoa maelekezo kwa Msajili Msaidizi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Bi. Dorothy Philip alipotembelea Banda la Msajili wa Mabaraza kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria inayoendelea jijini Dodoma

Maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma wakitoa huduma katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma.

***************************

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Katika kuhakikisha mlundikano wa mashauri ya migogoro ya ardhi unapungua nchini, Msajili wa Mabaraza ya Ardhi Stela Tullo ameelekeza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda kusikiliza mashauri katika wilaya nyingine ambazo hazina wenyeviti.

Akizungumza katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma Stela alisema, lengo ni kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati na haraka sambamba na kusogeza huduma karibu na wananchi.

‘’Katika kusogeza huduma karibu na wananchi tumeamua kusogezea huduma karibu wananchi ambapo tumejiwekea mikakati na kuelekeza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda wilaya nyingine ambazo hazina wenyeviti kusikiliza mashauri ya wananchi na siyo wananchi kuwafuata wenyeviti walipo’’. Alisema Stella

Kwa mujibu wa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya nchini Stella Tullo, kwa sasa kuna jumla ya Mabaraza 72 yanayotoa huduma na kati hayo Mabaraza 28 hayana wenyeviti waliopangiwa vituo katika wilaya hizo na kufanya wale wenyeviti wa wilaya za jirani kwenda kufanya kazi huko.

‘’Hivi sasa tuna jumla ya Mabaraza 72 na kati ya hayo 28 hayana wenyeviti hivyo kuna ratiba tumewapangia wenyeviti kwenda kusikiliza mashauri kwenye wilaya hizo jambo linalowapunguzia wananchi mzigo wa kusafiri kutoka wilaya moja kwenda nyingine.

Maonesho ya wiki ya sheria yalianza tarehe Januari 23, 2022 na kufunguliwa na Rais wa Zainzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Husein Ally Mwinyi na yanatarajia kufikia kilele siku ya jumamosi tarehe januari 29, 2022.

Post a Comment

0 Comments