Ticker

6/recent/ticker-posts

"SMZ INA MPANGO MADHUBUTI KUHAKIKISHA WANANCHI WANATUMIA BIDHAA ZENYE UBORA" MHE. HEMED


***********************

Kukamilika kwa Jengo la Ofisi na Maabara za Taasisi ya Viwango Zanzibar kutasaidia kuimarisha uwezo wa kiutendaji na kutoa huduma bora kwa watumiaji wa bidhaa, wazalishaji na wafanyabiashara kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameleeza hayo katika sherehe za ufunguzi wa Ofisi na Maabara za Taasisi ya Viwango huko Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mhe. Hemed amesema kuwa, Serikali ina mpango madhubuti katika kuhakikisha wananchi wake wanatumia bidhaa zilizo bora kwa lengo la kutunza Afya zao na mustakbali wa maisha yao.

Ameeleza kwamba, kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) Serikali itaendelea na hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa au kuingizwa nchini kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais amewataka viongozi na watendaji wa taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kuhakikisha wanapima sampuli za bidhaa zote pamoja na kutoa majibu kwa wakati sambamba na kuwa makini katika kufanya ukaguzi na udhibiti wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwa kutumia maabara hizo kwa kuwatumia wataalamu wa ndani. Amewakumbusha watendaji wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) kufanya kazi kwa bidii,ubunifu,uaminifu na kujiamini katika kusimamia majukumu ya kazi zao.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Hemed ametoa wito kwa wafanyabiashara wote Nchini kushirikiana kikamilifu na taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) ili kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa katika soko la Zanzibar zinakidhi matakwa ya viwango husika kwa lengo la kulinda Afya na usalama wa Mtumiaji.

Nae, Waziri wa Biashara Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaabani amesema nia na azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi ambapo ZBS ina mpango Kabambe wa kufanya mageuzi makubwa katika masuala ya ukaguzi na vipimo kwa bidhaa mbali mbali.

Amefafanua kwamba ndani ya kipindi cha muda mfupi ZBS imeshirikiana na taasisi tofauti za viwango katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR) Januari 09, 2022.

Post a Comment

0 Comments