Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) akiongea kuhusu nia ya Tanzania kuona Mkataba wa AfCFTA unakua chachu ya kuongeza fursa za kibiashara na uwekezaji wakati akishiriki Mkutano wa Nane wa Baraza la Mawaziri wa Biashara wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika, uliofanyika Accra, Ghana tarehe 28-29 Januari 2022.
..................................................
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) kwa niaba ya Serikali amelithibitishia Baraza la Mawaziri wa Biashara wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) nia ya Tanzania kuona Mkataba wa AfCFTA unakuwa chachu ya kuongeza fursa kwa nchi za Afrika kupanua zaidi biashara baina yao na kukuza uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Waziri Kijaji ameyasema hayo alipokuwa akishiriki Mkutano wa Nane wa Baraza la Mawaziri wa Biashara wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika, uliofanyika Accra, Ghana tarehe 28-29 Januari 2022. Waziri Kijaji aliongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano huo
Mkutano huo unaofuatia hatua muhimu ya Tanzania kuridhia na kujiunga katika Mkataba wa Kuanzisha Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kupitia Azimio la Bunge la Tanzania la Septemba 9, 2021 nakuifanya Tanzania kuwa nchi ya 40 kuridhia na kuwasilisha Hati ya Kuridhia Mkataba huo kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC). Amesema Waziri Kijaji.
Aidha, Mkutano huo uliohudhuriwa na nchi wanachama wa AfCFTA umejadili masuala muhimu yaliyosalia kuridhiwa ili kuwezesha biashara baina ya nchi za Afrika kuanza kufanyika chini ya Mfumo wa Eneo Huru la Biashara Afrika. Masuala hayo muhimu ni pamoja na ufunguaji wa biashara ya bidhaa, ufunguaji wa biashara ya huduma, vigezo vya uasili wa bidhaa, hakimiliki na bunifu, uwekezaji, pamoja na sera ya ushindani.Amesema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji ameeleza kuwa Baraza hilo la Mawaziri limeridhia kwa kauli moja mapendekezo ya hatua mbalimbali zilizopendekezwa ili kuharakisha mchakato wa kukamilisha majadiliano katika maeneo hayo yaliyobakia ili kutimiza kiu ya wadau wengi, hususan Sekta Binafsi barani Afrika kufaidika na uanzishwaji wa Eneo hilo lenye walaji takriban bilioni 1.3 linalotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kibiashara na kijamii barani Afrika.
Wakati huo huo, Akiwa Ghana, Waziri Kijaji amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Ghana Mhe. Alan Kyeremanten ambapo wamejadiliana namna ya kuanzisha mahusiano ya kimkakati ya kibiashara kati ya Tanzania na Ghana ili kuhakikisha uhusiano mzuri wa kisiasa na kihistoria uliopo baina ya nchi hizo mbili unakuwa na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania na Ghana.
Aidha, Katika kikao hicho Mawaziri hao walikubaliana pia kuchukua hatua za makusudi kuwaunganisha wadau wa Sekta Binafsi pamoja na wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kwa kuanzisha makubaliano rasmi na kuratibu ziara za mara kwa mara za kibiashara na kubadilishana utaalam na uzoefu katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Vilevile, Waziri Kijaji alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene, ambapo Katibu Mtendaji huyo alimpongeza kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa sekta muhimu ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa Sekretarieti katika kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa kikamilifu katika mchakato wa kukamilisha uanzishwaji wa Eneo hilo Huru la Biashara Afrika.
0 Comments