Ticker

6/recent/ticker-posts

MVUA ZA WASTANI HADI JUU YA WASTANI ZATARAJIWA KUNYESHA KUANZIA WIKI YA TATU HADI NNE MWEZI FEBRUARI KATIKA MAENEO MENGI NCHINI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa utabiri katika mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2022. Mtaalamu wa Hali ya Hewa TMA, Bi.Rose Senyagwa akitoa utabiri mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za TMA leo Jijini Dar es Salaam

********************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri katika mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2022 ambapo Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Akitoa utabiri huo leo Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt. Agnes Kijazi amesema Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mapema kati ya wiki ya tatu (3) na ya nne (4) ya mwezi Februari 2022 na kuisha mwezi Mei 2022 katika maeneo mengi.

"Ongezeko la mvua linatarajiwa hususan katika kipindi cha mwezi Machi 2022 katika maeneo ya pwani ya kaskazini na mwezi Aprili 2022 kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki". Amesema Dkt.Kijazi.

Amesema Mvua za Masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma ambapo mvua hizo zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari, 2022.

Aidha amesema Matukio ya magonjwa ya mlipuko na wadudu waharibifu yanaweza kujitokeza kutokana na hali ya unyevunyevu na kutuama kwa maji.

Pamoja na hayo amesema unyevunyevu wa udongo na maji kwa ajili ya umwagiliaji vinatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha kutosheleza mahitaji ya kilimo, malisho ya mifugo na wanyamapori.

Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji na afya kuendelea kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalam katika sekta husika.

Post a Comment

0 Comments