Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) katika Ofisi za Habari maelezo Jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Habari maelezo Jijini Dar es salaam
***************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imetoa maelekezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji zikiwemo za Mitaa katika mikoa mbalimbali nchini, ambazo ndizo zenye jukumu la msingi la menejimenti ya maafa, kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara yoyote yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za masika.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akitoa tamko la Serikali mbele ya waandishi wa habari jijini es Salaam kuhusu hatua za kuchukua wakati wa mvua za masika.
Balozi Dkt.Chana amesema kuwa, taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa Msimu wa Masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2022 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaonesha mvua hizo zitakuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.
Amesema, kutokana na hali hiyo, imeonekana kuna haja ya Serikali na wadau kuchukua hatua stahiki kuhakikisha matumizi bora ya mvua hizo pamoja na hatua za kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea.
Aidha ametoa wito kwa kila mwanachi, kaya pamoja na Kamati katika ngazi za mtaa au kijiji, wilaya na mkoa kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu katika suala zima la kushughulikia maafa kwa mujibu wa sheria ili msimu huu wa mvua usiathiri maendeleo ya taifa letu.
Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu shughuli za maafa kwa kuhakikisha ushiriki wa Wizara, Idara, Taasisi, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa, asasi zote zisizo za kiserikali pamoja na umma kwa jumla katika kuzuia, kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya Mwaka 2015
0 Comments