Zawadi kwa wanafunzi walioshiriki mdahalo huo zikitolewa.
Zawadi zikiandaliwa tayari kwa kutolewa.
**************************
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) kupitia mradi wa ‘AWARE 2020’ limewakutanisha Wanafunzi wa Shule za Sekondari ya Siuyu na Munkinya wilayani Ikungi Mkoani Singida katika mdahalo wa kujifunza mbinu bora za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Pamoja na mambo mengine wanafunzi hao walifanya mdahalo ili kupimwa uwezo wa kujieleza mbele ya umma na namna ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo Shule ya Sekondari Munkinya iliibuka kidedea.
Wanafunzi hao walikutanishwa na shirika hilo katika mdahalo huo uliofanyika jana wenye lengo la majadiliano kupitia Klabu ya Sauti za Wanafunzi (Student Voice Clubs-SVC) zilizoanzishwa na SPRF ili kupata ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimeanza kupungua kwa kiasi kikubwa baada ya shirika hilo na pengine kutoa elimu. mkoani hapa.
Mratibu wa Mradi kutoka SPRF, Mwalimu Bernard Maira alisema shirika hilo chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) limekuwa likitekeleza mradi wa AWARE katika shule wilayani humo kwa kufanya utetezi wa haki za wanawake na mtoto wa kike dhidi ya athari zitokanazo na mila na desturi kandamizi.
Alisema shirika hilo limewakutanisha wanafunzi hao na kufanya mdahalo huo ili kuwajengea uwezo kupitia klabu zao waweze kuwa na nguvu ya kupinga vitendo hivyo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
"Mafunzo tunayo wapa hawa wanafunzi yamewawezesha kupata nguvu ya kuelimisha umma pamoja na wazazi na walezi wao juu ya kupinga vitendo hivyo vyote vya ukatili wa kijinsiadhidi ya makundi hayo" alisema Maira.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ikungi, Haroun Yunus Haroun alisema mdahalo huo waliouendesha kwa wanafunzi hao ulilenga kuwapa uwezo wa kujieleza na kujiamini.
"Mashindano haya kupitia mdahalo huu tumeyafanya si kwa lengo la kuona kundi lingine halifai bali yote ni sawa na kuwa yanalenga kuwajengea uwezo wanafunzi hao wa kujiamini na kuwa na ujasiri wakati wa kufuatilia masuala yote ya ukatili" alisema Haroun.
Mmoja wa Wanafunzi wa Sekondari ya Munkinya wa klabu ya SVC alisema baada ya kupata mafunzo hayo nao uenda kuwafundisha wenzao na jamii na wanapopata taarifa ya matukio ya ukatili huyapeleka SPRF kwa hatua zaidi.
Mwanafunzi huyo alisema mafunzo hayo wanayopatiwa na shirika hilo yanawaongezea ari ya kupata uelewa zaidi na kujiamini katika kukabiliana na vitendo hivyo.
Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Siuyu wa klabu hiyo alisema wamekuwa wadau wakubwa wa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na mara baada ya kupokea taarifa za matukio hayo wamekuwa wakiziwasilisha maeneo husika kwa hatua zaidi za kisheria.
"Tukiyabaini matukio ya ukatili wa kijinsia tunatoa taarifa kwa walimu walezi ambao nao waliyapeleka ngazi za kata jambo linalosaidia kupunguza kwa vitendo vya ukatili" alisema.
Zawadi zilizotolewa kwa wanafunzi walioshinda kwenye mdahalo huo ni cheti kwa mshindi wa kwanza, cheti kwa mshindi wa pili na madaftari kwa washiriki wote na kwa mwanafunzi kinara aliyefanya vizuri zaidi kuliko wengine, Anna Selemani kutoka Shule ya Sekondari ya Siuyu alizawadiwa fulana.
Tangu shirika hilo lianze kutoa mafunzo ya kukabiliana na mambo ya unyanyasaji wa watoto na wanawake vikiwemo vitendo vya ukeketaji, mimba,ndoa za utotoni na ubakaji matukio hayo yameanza kupungua.
0 Comments