Mkurugenzi wa Asasi ya SIREWOCHA GROUP-Tanzania Enock Mwang’onda akizungumza na vyombo vya habari kwenye makao makuu ya Asasi hiyo iliyopo Manispaa ya Singida mkoani hapa hivi juzi.
Mkurugenzi wa Asasi ya SIREWOCHA GROUP-Tanzania Enock Mwang’onda akiwa kwenye makao makuu ya ofisi hiyo.
Mwonekano wa jengo la utawala la makao makuu ya ofisi hiyo.
Bango la anuani ya ofisi lililopo nje ya jengo la makao makuu ya ofisi hiyo.
***************************
Na Godwin Myovela, Singida.
ASASI isiyo ya kiserikali ya Sirewocha Group-Tanzania yenye makao yake makuu ndani ya Manispaa ya Singida mkoani hapa tayari imeanza rasmi zoezi la kusajili makundi ya wastaafu, wazee, walioachishwa kazi kisheria na wote wenye mahitaji maalum maarufu ‘ombaomba’ ili kuwaunganisha pamoja na kuanza kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo fedha taslimu na vifaa mbalimbali vya kujikimu kimaisha badala ya kuendelea kuzurura hovyo mitaani
Kwa mujibu wa Sirewocha pamoja na mambo mengine, zoezi la ugawaji wa fedha na vifaa mbalimbali ikiwemo nguo na vyakula kwa wahitaji, simu za mkononi kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano, fimbo za kuwaongoza wasioona sambamba na kusajili watoto wa mitaani ili kuwapatia misaada na kuwarejesha makwao kwa kuwaunganisha na wazazi wote watakaokuwa na nia hiyo-kwa kila siku za Ijumaa-litaanza Februari 4 mwaka huu.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani hapa jana, Mkurugenzi wa Asasi hiyo Enock Mwang’onda alisema asasi hiyo baada ya mkoa wa Singida inatarajia kusambaza huduma hiyo kwa kuweka ofisi zake Tanzania Bara, lengo ni kuhakikisha wanafanikiwa kuondoa ombaomba wote mitaani kwa kuanzia na mkoa wa Singida na kuwaunganisha wote wenye mahitaji mapema ifikapo 2025.
“Tayari tumewawekea ofisi yao hapa ambayo watakuwa wakikutana hapa kwa kila siku za ijumaa kuanzia ijumaa ijayo (Februari 4) kupata misaada mbalimbali…lengo letu hasa ni kurudisha hadhi na kuwajengea heshima inayostahili hawa wenzetu badala ya kuwaacha tu wakiendelea kuombaomba mitaani,” alisema Mwang’onda
Asasi hiyo iliyosajiliwa Oktoba 29 mwaka jana ndani ya Manispaa ya Singida, pamoja na mambo mengine inatarajia kusaidia pia makundi mengine ya wahitaji, ikiwemo kuwanunulia sare za shule watoto yatima, kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali kwa wastaafu ili kuwapunguzia ukali wa maisha-sanjari na kuwafikia wazee na vikongwe.
“Kwa kuwa lengo letu ni kusaidia watu wenye mahitaji maalumu tunawaomba watanzania wote wenye mapenzi mema na watakaoguswa na namna tunavyotoa huduma hii kutuunga mkono kwa kuleta michango yao ya hali na mali kwenye ofisi yetu ili tuwagawie wahitaji wa makundi haya, alisema Mwang’onda.
0 Comments