Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akisisitiza jambo wakati wa kufunga kikao kazi cha Menejimenti, Wakurugenzi Wasaidizi na Makamishna wa Ardhi wa mikoa kilichofanyika mkoani Arusha Tarehe 26 Februari 2022. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi cha Menejimenti, Wakurugenzi Wasaidizi na Makamishna wa Ardhi wa mikoa kilichofanyika mkoani Arusha Tarehe 26 Februari 2022.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi cha Menejimenti, Wakurugenzi Wasaidizi na Makamishna wa Ardhi wa mikoa kilichofanyika mkoani Arusha Tarehe 26 Februari 2022.
Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nhonge akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi cha siku mbili cha Menejimenti, Wakurugenzi Wasaidizi na Makamishna wa Ardhi wa mikoa kilichomalizika tarehe 26 Februari 2022 mkoani Arusha.
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha Menejimenti, Wakurugenzi Wasaidizi na Makamishna wa Ardhi wa mikoa wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (hayupo pichani) wakati wa kufunga kikao hicho cha siku mbili mkoani Arusha Tarehe 26 Februari 2022.
*****************
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanazingatia utoaji huduma bora kwa wateja ili kuondoa malalamiko kwa wanaokwenda kupata huduma kwenye ofisi za ardhi.
Aidha, Ridhiwani aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma zao na kuacha kufanya kazi kwa kisingizo cha kutekeleza maagizo ya wanasiasa.
Naibu Waziri Ridhiwani alisema hayo tarehe 26 Februari 2022 wakati akifunga kikao kazi cha Menejimenti, Wakurugenzi Wasaidizi wa Wizara ya Ardhi pamoja na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa kilichofanyika mkoani mkoani Arusha.
‘’Wakati mnafikiria kutoa huduma kwa wananchi wetu, ‘customer care’ ni jambo la muhimu sana maana yapo baadhi ya malalamiko kutoka kwa wananchi wetu kuhusu ucheleweshaji wa makusudi wa kupatiwa huduma, suala ambalo kama watendaji wakuu tulipaswa kulishughulikia’’ alisema Ridhiwani.
Akitolea mfano wa mama mmoja aliyemfuata akimlalamikia kukwama kupatiwa hati yake kwa muda mrefu, Ridhiwani alieleza kuwa baada kufuatilia kwa kumpigia simu afisa ardhi kwenye halmashauri husika kuhusiana na malalamiko hayo aliambiwa kuwa, mama huyo hakuwasilisha kitambulisho cha taifa jambo lililomfanya kuhoji ni nani anayepaswa kumpa taarifa mama huyo kwa kuwa taarifa za kitambulisho alipewa yeye na siyo mama mhusika.
Alisema, wizara ya Ardhi inapotaka kukusanya vizuri mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi basi chanzo chanzo ni utoaji hati za ardhi kwa kuwa wanaopatiwa hati wanakuwa sehemu ya walipa kodi. Kwa mujibu wa Ridhiwani, iwapo Wizara haitapima, kupanga na kutoa hati basi kila siku jukumu lake iitakuwa kukumbushana wajibu wa kukusanya mapato wakati uwezekano wa kufikia malengo haupo kutokana na miundombinu iliyopo.
Aliwataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kusisitiza kwa maafisa ardhi wa halmashauri za wilaya, manispaa na majiji kutambua umuhimu wa kufanya kazi sambamba na kutambua kufanya kazi na watu kwa lengo la kuwa karibu ili kuwafanya wafurahi, wapate hati na kupimiwa maeneo yao.
Akigeukia suala la utendaji kwenye kwa watendaji wa sekta ya ardhi, Ridhiwani aliwataka watendaji wa sekta hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia taaluma zao na kuacha kufanya kazi kwa kisingizio cha kutekeleza maagizo ya wanasiasa.
‘’Msije kutugeuza viongozi wenu kuwa kivuli cha kujitetea katika utendaji kazi wenu, nawaombeni sana na maagizo haya myashushe mpaka kwa maafisa ardhi katika halmashauri, wasifanye vitu vya ovyo kwa visingizio vya wanasiasa’’ alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema, kupitia kikao kazi waliweza kujadili mapungufu na kubainisha mikakati itakayosaidia kuondoa mapungufu ya kiutendaji.
Alisisitiza umuhimu wa viongozi wa idara na Makamishna wa Ardhi wa mikoa kuwa wepesi katika kufanya maamuzi na kubainisha kuwa, mara nyingi kumekuwa na mzingo kazi unaosababishwa na ulimbikizaji wa kazi na kutaka kuwepo mkakati wa kumaliza au kuondoa kazi za nyuma na zile zinazojitokeza.
‘’Ni muhimu kuwa wepesi katika kutoa maamuzi na kila mmoja anayefanya kazi afikirie ‘Real time solution’ maana mara nying tunakuwa na mzigo wa kazi kutokana na kulundika kazi na ili kuondoa mzigo huo tushughulikie za nyuma na zile zinazojitokeza’’ alisema Dkt Kijazi
0 Comments