Ticker

6/recent/ticker-posts

MAAFISA UTUMISHI WAPATA ELIMU YA FIDIA KWA WAFANYAKAZIMAAFISA UTUMISHI WAPATA ELIMU YA FIDIA KWA WAFANYAKAZI

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, ARUSHA.

Maafisa Utumishi na Utawala kutoka halmashauri mbalimbali nchini wamekumbushwa kuwa moja ya majukumu yao ni kuwasilisha taarifa WCF kwa wakati za watumishi kunapotokea ajali au ugonjwa kutokana na kazi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Utumishi kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Shinyanga Machi 21, 2022, jijini Arusha, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini kutoka WCF Dkt. Abdulssalaam Omar amesema “WCF inakidhi matakwa ya mikataba ya kimataifa kuhusu Fidia kwa wafanyakazi ambapo kukuza mbinu za kuzuia ajali na magonjwa kutokana na kazi ni moja ya matakwa hayo.” Alifafanua Dkt. Omar.

Amewaambia washiriki kuwa Mfuko umekuwa na faida kubwa kwa wafanyakazi, waajiri na Taifa kwa ujumla kwani wafanyakazi wana uhakika wa kinga ya kipato kutokana na majanga yasababishwayo na ajali na magonjwa kutokana na kazi.

Amesema zaidi ya Wafanyakazi kuwa na uhakika wa kinga ya kipato, kadhalika waajiri nao wanapata muda zaidi wa kushughulikia masuala ya uzalishaji na uendelevu wa biashara zao kwani Mfuko ndio unaobeba jukumu la kugharamia pindi mfanyakazi anapoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi. Alisisitiza.

Lakini pia "Wafanyakazi nao wanapata utulivu kazini kutokana na kupungua kwa migogoro hata pale ajali zinapotokea sehemu za kazi na hii inasaidia sana kuongeza tija na uzalishaji na kuchangia kuongeza pato la taifa.

Aidha alidokeza kuwa ili kuhakikisha Sekta Binafsi inaendelea kushamiri Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewapunguzia mzigo Waajiri wa sekta binafsi kwa kuelekeza punguzo la uchangiaji kuanzia mwezi Julai mwaka huu ambapo wanachangia katika Mfuko wa Fidia asilimia 0.6% badala ya asilimia 1% ya mapato ya wafanyakazi wao.

"Si hivyo tu hata riba (interest) kwa michango iliyochelewa imepungua kutoka asilimia 10% ya kila mwezi kwa malimbikizo ya deni la nyuma hadi kufikia asilimia 2% tu," alisema.

Wakati wa Mafunzo, Maafisa Utumishi hao walijifunza pamoja na mada nyengine mbinu za kuzuia ajali kazini mada iliyowasilishwa na Meneja tathmini za vihatarishi kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bi. Naanjela Msangi aliyesema Waajiri hawana budi kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa kuwapatia wafanyakazi vifaa vya kujikinga (Protective gears) na wahakikishe wanavitumia ipasavyo wanapotekeleza majukumu yao ya kazi ili kuwakinga na ajali zitokanazo na kazi.

Mada nyengine zilizowasilishwa na timu ya WCF zilikuwa ni pamoja na namna ya kutoa taarifa WCF za matukio ya ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi kupitia Mtandao-Online Notification System (ONS) na zaidi ya hayo, kulikuwepo na mada nyingine kuhusu Mafao ya Fidia yatolewayo na WCF.

Wakati wa mafunzo hayo, timu ya WCF iliongoza washiriki katika mazoezi kwa vitendo ambapo washiriki walipangwa kwenye makundi na kujifunza mambo mbalimbali ya kiutendaji kuhusiana na madhara yanayotokana na kazi, hatua za kuchukua, uwasilishaji wa taarifa kwa njia ya mtandao, matumizi ya huduma zitolewazo na WCF na masuala mengine ya muhimu kuhusu Fidia kwa Wafanyakazi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata mafunzo hayo, washiriki wamesema mafunzo yamekuwa ni yenye manufaa makubwa sana kwao na bila shaka watatumia elimu waliyoipata ili kuhakikisha wanatekeleza vema jukumu la kuzuia ajali na magonjwa kutokana na kazi kwa wafanyakazi lakini pia kuwaelimisha wenzao hatua za kufuata pindi wanapokumbwa na majanga kama ajali na magonjwa kutokana na kazi.

“Elimu hii imeniongezea uelewa kuhusu masuala ya fidia lakini pia hatua anayopaswa kuchukua mfanyakazi pindi anapoumia, kuugua au kinapotokea kifo kutokana na kazi." Alisema Sylvia Mtweve, Afisa Utumishi kutoka Tanga.

Alisema katika jiji la Tanga tayari amesimamia utaratibu wa wafanyakazi zaidi ya 10 kuwasilisha madai yao, ambao walipatwa na majanga mbalimbali yatokanayo na kazi na wote wamepatiwa fidia na WCF.

Naye Bw. Policarp Mpulumba, Afisa Tawala kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema mafunzo hayo yamewakumbusha kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa bora zaidi.


Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar, akiwasilisha Mada ya Mafao ya Fidia yanayotolewa na WCF.


Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka TAMISEMI-Dodoma, Bi. Joyce Mushi, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Bi. Naanjela Msangi, Meneja Tathmini ya Vihatarishi Mahala pa Kazi, kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), akiwasilisha mada ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi.
Kaimu Afisa Mfawidhi WCF, mkoa wa Arusha, Kanda ya Kaskazini Bw. Joseph Joseph Siri (kulia), akifuatilia majadiliano ya vikundi ya washiriki wa mafunzo hayo.
Afisa Mwandamizi Idara ya Tathmini WCF, Bw. Robert Duguza, akiwasilisha Mada ya namna ya kutoa taarifa Kupitia mtandao (Online Notification System-ONS).

Washiriki wakiwa Mafunzoni.

Washiriki wakiwa Mafunzoni



Baadhi ya washiriki.
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini, Dkt. Abdulsalaam Omar (katikati) akifuatilia majadiliano ya vikundi kuhusu visa mbalimbali vya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi na namna ya kutoa taarifa kwenye Mfuko.
Maafisa Waandamizi wa WCF, Bi Amina Likungwala (kushoto waliosimama) na Bi. Tumaini Kyando wakisikiliza majadiliano ya vikundi kuhusu visa halisi vya ajali na magonjwa yatokanayo na Kazi na namna ya utoaji taarifa.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Bi. Laura Kunenge (aliyesimama) akisikiliza kwa makini mwenendo wa majadiliano ya vikundi.
Majadiliano yakiendelea.



Post a Comment

0 Comments