*****************
Na. John Mapepele
Nahodha wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu wa Tanzania Mbwana Sammata na mamia ya watu maarufu wamejitokeza kuchangia timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars katika kuadhimisha Siku ya wanawake duniani kwenye tamasha la The Orange Concert Machi 8, 2022 jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusu tamasha hilo leo Machi 7, 2022 Sammata amesema anaipongeza Serikali kupitia Wizara Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu wa kuandaa tamasha hilo la kihistoria kwenye siku ya mwanamke duniani kuwachangia Twiga star ili waweze kuendelea kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
"Mimi Mbwana Sammata Nahodha wa Timu ya Taifa natambua kazi kubwa wanayofanya dada zetu wa Twiga Stars katika ramani ya michezo naungana na Serikali yangu nikisema tano kwa Twiga Stars katika tamasha hili la The Orange Concert " amesisitiza Sammata
Ametoa wito kwa watanzania wote kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassani za kuendeleza michezo kwa kuwachangia Twiga Star ambapo amesema wanawake wamekuwa wakifanya vizuri hivyo jamii ina wajibu wa kuwasaidia kwa hali na mali ili wafanye vizuri na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa katika michezo.
Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Dada Hood inayojishughulisha na kupinga unyanyasaji wa kijinsia wameandaa Tamasha la kuichangia timu ya wanawake Twiga Stars.
Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema siku hiyo imeratibiwa maalum kwa ajili kufanya harambee kuichangia timu ya wanawake Twiga Stars ikiwa ni mkakati madhubuti ya kuendeleza michezo kwa wanawake hapa nchini.
"Sisi kama wizara yenye dhamana na michezo katika siku ya wanawake nchini tumekuja na kitu cha tofauti tunaipongeza Twiga Star lakini tuna hamasisha wadau na wapenda michezo wote nchini kuichangia ili tuinue michezo kwa wanawake hapa"
Dkt. Abbasi amesema Tamasha hilo litakalofanyika Siku ya Wanawake Duniani litapambwa na wasanii wa kike 10 ambapo wasanii wa kiume pia wamemiminika kwa wingi kutoa support kwa wanawake katika tamasha hilo la kihistoria.
Tamasha hili limeibua hisia kali kwa wadau mbalimbali ambapo wamekuwa wakipongeza Serikali kwa kuandaa tamasha hili huku wakiahidi kushiriki na kuwachangia wanawake kwa kuwa wamekuwa wakiiwakilisha vizuri Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewapongeza taasisi ya Dada Hood kwa kazi zao za kuwainua watoto wa kike hasa nia yao ya kuichangia timu ya wanawake ya Taifa Twiga Satars.
Msitha ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia sekta ya michezo kwa upande timu za taifa za wanawake ambazo zinaendelea kupeperusha vema bendera ya taifa kimataifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake (TWFA) Somoe Ng'itu ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Dada Hood na kuwakaribisha wadau wengine kuendelea kuwashika mkono Twiga Stars ili waendelee kuliheshimisha nchi kimataifa.
0 Comments