Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YALETA MFUMO MPYA KWA MASHIRIKA, VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika yaliyobinafsishwa leo jijini Dar es Salaam kilicholenga kubadilishana mawazo katika usimamizi na uendelezaji wa taasisi hizo kwa maslahi mapana ya nchi, hasa ikizingatiwa kuwa pamoja na mambo mengine, ubinafsishaji ulilenga kuongeza uzalishaji, ufanisi na tija, kuongeza mapato kwa Serikali, kuingia teknolojia ya kisasa na kushirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi. Wengine picha ni Mkurugenzi wa Ubinafsishaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama na Neema Musomba, Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti katika Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina). Sehemu ya wamiliki na wakurugenzi wa mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa ambao jana walijitokeza katika kikao kazi kati yao na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto leo jijini Dar es Salaam ili kubadilishana mawazo katika usimamizi na uendelezaji wa taasisi hizo, lengo likiwa kutaka kuhakikisha malengo ya ubinafsishaji yanafikiwa. Kikao kama hicho kilifanyika pia Dodoma wiki iliyopita. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika yaliyobinafsishwa mara baada ya kikao kazi baina yao hivi karibuni jijini Dodoma kilicholenga kubadilishana mawazo katika usimamizi na uendelezaji wa taasisi hizo kwa maslahi mapana ya nchi, hasa ikizingatiwa kuwa pamoja na mambo mengine, ubinafsishaji ulilenga kuongeza uzalishaji, ufanisi na tija, kuongeza mapato kwa Serikali, kuingia teknolojia ya kisasa na kushirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina). Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza katika kikao kazi chake na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa hivi karibuni jijini Dodoma. Kikao kama hicho kilifanyika tena leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Ubinafshaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama wakati wa kikao kazi na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa hivi karibuni jijini Dodoma. Kikao kama hicho kilifanyika tena leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).


Wawekezaji Leby Gabriel, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chai Wakulima ya Rungwe mkoani Mbeya na Katherine Mwimbe wa Domya Estate ya Dodoma iliyochukua kiwanda cha Dodoma Wine, wakibadilishana nyaraka wakati wa kikao kazi baina ya Msajili wa Hazina na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa. Kikao kazi hicho kilifanyika hivi karibuni jijini Dodoma. Aidha, kikao cha aina hiyo kilifanyika pia leo Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina mara baada ya kikao kazi kati yake na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa, leo jijini Dar es Salaam. Wengine pichani waliokaa ni Mkurugenzi wa Ubinafsishaji, Mohammed Nyasama na Pili Mazowea, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu.

(Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)

***********************

*Yalenga kufuatilia mafanikio, changamoto za wawekezaji

 *Yasisitiza ubinafsishaji ulilenga kuongeza tija, ufanisi

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inakamilisha mfumo rahisi wa kupokea na kutunza kumbukumbu za Mashirika ya Umma na Viwanda vilivyobinafsishwa unaoitwa Ubinafsishaji Information System ili kuweza kufuatilia mafanikio na changamoto za mashirika na viwanda hivyo.

Hayo yamesemwa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto wakati wa kikao kazi kati yake na wamiliki na wakurugenzi wa mashirika hayo ya umma yaliyobinafsishwa kilichofanyika jijini Dar es Salaam leo, ikiwa ni mwendelezo wa kikao kingine cha aina hiyo kilichofanyika wiki iliyopita jijini Dodoma.

Alifafanua kuwa, mashirika hayo ya umma yalibinafsishwa ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuyaendesha ikiamini kwa kufanya hivyo yangeongeza tija na ufanisi ikiwamo uingizaji wa teknolojia mpya, lakini kubwa zaidi, Serikali ililenga kuishirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi.

Msajili wa Hazina Mgonya alisema mfumo huo upo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji na kwamba utakapoanza kutumika wawekezaji watateua maofisa wao watakaokuwa na jukumu la kutoa taarifa husika na kusaidia kupunguza safari za maofisa wa serikali kutembelea waliouziwa mashirika hayo.

Mashirika takribani 200 kati ya yaliyobinafsishwa, yalifuatiliwa na kufanyiwa tathmini katika mwaka 2021. Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, kati ya hayo yaliyofuatiliwa imebainika ni mashirika 76 tu yanayofanyakazi vizuri, 41 yanasuasua na 83 hayafanyi kazi na yamefungwa. Aidha kati ya mashirika hayo, viwanda vilikuwa 108, mashamba 54, hoteli 19 na kampuni 19.

Alisema tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na wawekezaji kuboresha utendaji wa mashirika hayo.

Ikiwa ni mara ya kwanza kwa Msajili wa Hazina kukutana na wawekezaji wa Mashirika yaliyobinafishwa ili kubadilishana mawazo katika usimamizi na uendelezaji wa taasisi hizo kwa maslahi mapana ya taifa, Mgonya alisema serikali katika kubinafsisha mashirika, viwanda, mashamba na hoteli ilikuwa na lengo la kuongeza uzalishaji, ufanisi na tija.

Msajili wa Hazina hata hivyo amewatoa shaka wamiliki na wakurugenzi wa mashirika na viwanda hivyo na kusema kwamba wanachofanya wao sio kupanga kuwapora viwanda na mashirika yao, bali kuona kwamba makubaliano yanatekelezwa kwani katika ufuatiliaji pia wamebaini kuwepo kwa kasoro mbalimbali ikiwamo wamiliki kukopa fedha kwa shughuli nje ya uendelezaji wa mashirika yenyewe.

Alisema tangu Ofisi ya Msajili wa Hazina iliporithi majukumu ya lililokuwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) mwaka 2014 wamekuwa wakitakiwa kufuatilia na kufanya tathmini ili kuona maendeleo ya mashirika na kampuni hizo.

"Mategemeo na malengo ya kubinafsisha yalikuwa pia kuongeza mapato kwa Serikali na kuipunguzia Serikali mzigo wa kuyahudumia mashirika hayo, kuingiza teknolojia ya kisasa katika uendeshaji wa mashirika hayo, na kubwa zaidi ni kuishirikisha sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi hasa katika maeneo ambayo Serikali haijafika" alisema Msajili Mgonya.

Alisema kutokana na mazingira hayo, serikali inapofanya ufuatiliaji na tathmini haina maana ya Serikali kutaka kupokonya mali iliyouzwa au kutaka kuifanya kampuni ilipe kodi kubwa kinyume na sheria, kanuni na taratibu za nchi, bali kubaini changamoto na kusaidia njia za kuzikabili.

Aliwataka wawekezaji hao waliouziwa mashirika, mashamba, hoteli na viwanda vilivyokuwa vya Serikali watoe ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina wakati inapofanya Ufuatiliaji na Tathmini ili kwa pamoja changamoto zibainike na njia ya kuzikabili kutafutwa kwa pamoja.

"Lengo likiwa ni kutambua ikiwa malengo ya Serikali ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma yamefikiwa. Aidha, pale itakapobainika kuna changamoto zinazopelekea malengo ya ubinafsishaji kutofikiwa hatua stahiki huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kurekebisha mikataba ya mauziano pamoja na mipango ya uwekezaji iliyokubaliwa wakati wa ubinafsishaji" alisema.

Mwaka 1993 Serikali ilianzisha PSRC na kuipa jukumu la kushirikiana na Sekta binafsi kurekebisha na kufufua mashirika ya umma yaliyokuwa yanaendeshwa kwa hasara.

Hiyo ilitokana na Serikali kuanza kutekeleza mpango wa ubinafsishaji na urekebishaji wa Mashirika ya Umma mwishoni mwa mwaka 1992 baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Mashirika ya Umma SURA 257, lengo likiwa kuruhusu sekta binafsi na Watanzania wengi waweze kushiriki katika kumiliki na kuendesha Mashirika ya Umma ambayo kwa wakati huo yalikuwa hayafanyi vizuri.

Njia zilizotumika katika kurekebisha mashirika hayo ni pamoja na Uuzaji wa mali (Asset Sales), Uuzaji wa hisa (Share Sales), Ushirikishaji wa Sekta binafsi (Joint Venture- Partnership), kukodisha (Leasing), Shirika au kampuni kuuzwa kwa wafanyakazi (Management and Employment Buy Out – MEBO) na ufilisi.

Post a Comment

0 Comments