Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt.Jabir Bakari akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusiana na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka hiyo katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahariri na watumishi wa TCRA katika mkutano wa kuangalia mafanikio ya utoaji huduma za Data Mkurugenzi wa masuala ya Kisekta wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Emmanuel Manase akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari ,jijini Dar es Salaam.
********************
Na Mwandishi wetu
“KATIKA orodha ya mataifa yaliyo na bei ya chini ya bandle ‘kifurushi’ sisi Tanzania tumo. Si Afrika wala duniani sisi tumo tukiwa na viwango vya chini zaidi.”
Hii ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabir Bakari anayoitoa katika kikao baina ya mamlaka hiyo na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kubadilisha mawazo ambapo viongozi mbalimbali wa mamlaka hiyo, walielezea masuala mbalimbali na wahariri kuulizwa maswali na kutoa ushauri kadhaa wenye lengo la kuboresha.
Katika wasilisho lake kwa wahariri lililojikita zaidi kuelezea gharama za vifurushi ‘bando’ Dk. Bakari anasema kwa tafiti nyingi za Kimataifa zilizofanywa na amshariki kadhaa, zinaonesha Tanzania inaongoza kuwa na gharama nafuu za mawasiliano ya simu na data Afrika na duniani.
Anasema, wastani wa gharama za data nchini ni takribani senti 75 za kimarekani kwa Gigabaiti moja ya data ambapo kwa mujibu wa taasisi ya Cable.co.uk ya Uingereza, ndio bei rahisi zaidi katika eneo zima la Afrika Mashariki na kati.
Mkurugenzi mkuu huyo anasema, Tanzania ni nchi ya sita kati ya nchi 52 kwa unafuu wa bei za data barani Afrika kwa mujibu wa utafiti uliofanywa wa taasisi ya Techcabal Afrika.
“Huu utafiti upo mtandaoni, mtu yeyote akiuhitaji anaweza kuingia kwenye tovuti yao na kuusoma. Kuwa nchi ya sita kati ya 52 si jambo dogo, Serikali inajitahidi sana kuwalinda wananchi wake,” anasema
Aidha, Dk. Bakari anasema, Tanzania pia imebainika kuwa ni nchi ya 21 kati ya nchi 155 kwa unafuu zaidi wa gharama ya mawasiliano ya simu na data duniani kwa mujibu wa utafiti wa Kimataifa, uliofanywa na Visual –capitalist worldwide mobile data, 2021.
“Tanzania pia ni nchi ya 32 kati ya nchi 230 kwa unafuu zaidi wa bei za data kwa mujibu wa taasisi nyingine ya utafiti ya Kimataifa ya Cable worldwide data,” anasema Dk. Bakari
“Hivyo basi, Tanzania inashika nafasi ya 32 duniani miongoni mwa nchi za gharama za chini zaidi za data kwa ajili ya Intaneti. Hii ni kutokana na utafiti uliofanywa na Cable.co.uk,” anasisitiza
Anasema, upatikanaji wa gharama nafuu za data kwenye simu ni miongoni mwa mafanikio ya Serikali ambapo tafiti kadhaa zimebainisha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye gharama nafuu na ya chini ya data.
Mathalani, bei ya data kwa wastani wa 1GB ni Dola za Kimarekani (USD) 0.750 sawa na Sh.1,725.
“Barani Afrika Tanzania imo miongoni mwa nchi sita kinara kwa unafuu wa gharama ya data inayotumika kwenye simu,” anasema
Akisisitiza katika eneo hilo, Dk. Bakari anasema “hatua hii ni muhimu ikizingatiwa Serikali imekuwa ikiweka mazingira wezeshi ya uwepo wa watoa huduma wengi wa mawasiliano ya simu.”
Anasema uwingi wa kampuni za utoaji huduma za simu umeleta ushindani ambao sasa unawezesha kushusha bei za mawasiliano ya simu pamoja na data.
“Kati ya mwaka 2015 na Februari mwaka huu bei ya mawasiliano ya simu zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 88 kwa mujibu wa TCRA,” anasema
Anasema katika eneo la Afrika Mashariki, Tanzania imeziacha mbali nchi jirani za Congo, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Malawi, Zambia pamoja na Msumbiji.
Tafiti za Kimataifa pia zimebainisha nchi za Congo na Kenya ndio zenye gharama kubwa zaidi kwa Afrika Mashariki, huku Malawi ikiwa na gharama kubwa kupita nchi zote za kusini mwa afrika.
Katika kikao hicho, mmoja wa wahariri alitaka kujua kama laini zote za simu zimesajiliwa, kwa nini bado kuna watu wanaotuma ‘sms’ zenye jumbe za kitapeli ikiwemo kujiunga na Freemason?
Akijibu kwa kifupi, Dk. Bakari anasema, “tuko kazini kwenye hilo tuacheni.”
Aidha, mkurugenzi huyo anasema, hadi kufikia Desemba mwaka jana, laini zote za simu zilikuwa zimesajiliwa “kwa hiyo hakuna uhalifu unaoweza kufanyika tusimjue. Laini zote zimesajiliwa na kama kuna changamoto mbalimbali, tunazifanyia kazi.”
Vifurushi kuisha haraka
Katika mkutano huo, kuliibuka hoja ya vifurushi kumalizika haraka ambapo Dk. Emmaniel Manase, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA akabainisha mambo yanayoweza kusababisha tatizo hilo ambalo baadhi ya wananchi hawalifahamu.
Dk. Manase akabainisha kwamba, vifurushi vinaweza kuisha mapema kutokana na kuongezeka kwa kasi ya mitandao na simu janja ‘smartphone.”
Anasema, unakuta simu ilikuwa na laini ya 3G, ukahamia 4G, “sasa wakati anafurahia simu ina pakua haraka inakula kwa kasi vifurushi na si kasi tu ubora wa video na picha inaongezeka, “ubora wa hayo unapoongezeka na matumizi ya bando yanaongezeka.”
Jambo jingine anasema, simu janja zinapokuja, “oparetion system zinaongezeka, zinakuwa kubwa na zamani ulikuwa unatumia 2GB kufanya update, lakini tunatumia application nyingi sana na hizi zinafanyiwa update mara kwa mara na Watanzania walio wengi hatuna njia nyingine kutumia intanet nje ya simu zetu.”
Dk. Manasema anasema, watumiaji wengi wa simu, unakuta inapakua background bila wewe kujijua. Lakini uwepo wa application nyingine ambazo hazitumii na zinaongeza matumizi ya data.
Ili kukabiliana na tatizo hilo na kuwasaidia watumiaji, Dk. Manasema anasema, “tumewaelekeza watumiaji wa huduma kuandaa application kuonesha umebakiza sms, data na dakika ngapi, ili mtumiaji wa simu awe anaona kile anachokitumia.”
0 Comments