***************************
Na Eleuteri Mangi-WUSM, Dodoma
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake imejipanga kutekeleza maelekezo 16 ya kisekta kwa kasi na weledi katika mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuwahudumia wananchi.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Machi 21 Jijini Dodoma wakati akiwa mgeni rasmi kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa mwaka 2022 ambapo wizara imedhamiria kuyatekeleza kwa ufanisi kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanaitegemea wizara hii kwa namna moja au nyingine.
Mhe. Mchengerwa amesema maelekezo hayo yametolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa ambayo lengo lake ni kuwahudumia Watanzania.
“Kila mmoja awajibike kwenye eneo lake, tukijifungia ofisini hatutafikia malengo na matarajio ya Serikali, twende kuwahudumia wananchi, tuwafikie na kuwapa faida ya Serikali yao”. amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Miongoni mwa maelekezo ya viongozi hao ni kuhakikisha matamasha ya Utamaduni nchi nzima yanafanyika katika ngazi za wilaya hadi mtaa na washindi kupewa zawadi, kuimarisha usimamizi wa masuala ya haki miliki ili wasanii waweze kunufaika na kazi zao, kuanzisha na kuwezesha shule 56 za Tanzania Bara kuwa maeneo ya academia za michezo, kukamilisha mapitio ya Sera zinazohusu sekta za wizara, kutangaza nchi kupitia michezo na utalii, kukuza na kuendeleza sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili iendelee kutengeneza fursa za ajira na kuimarisha usimamizi wake.
Pia amesema wizara imeelekezwa kujenga miundombinu ya kisasa ya michezo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa soka wa Dodoma ambao unatarajiwa kuchukua mashabiki 100,000, kujenga kituo maalum cha kulea vipaji vya michezokatika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, kujenga viwanja vitatu vya kisasa vya mazoezi na kupumzikia wananchi katika mikoa ya Dar es Salaa, Dodoma na Geita, kujenga kumbi kubwa kwa ajili ya michezo na maonesho ya Sanaa utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 15,000 katika mikoa ya Dar es salaam na Dodoma na kugharamia maandalizi.
Maelekezo mengine ni pamoja na kugharimia maandalizi na ushiriki wa Timu za Taifa za wanawake huku akitolea mfano timu ya Serengeti Girls ambao wameendelea kufanya vizuri kuelekea kufuzu michuano ya kombe la dunia kwa kuifunga timu ya Botswana kwa goli 4-0.
Kwa upande mwingine Mhe. Mchengerwa amesema wizara yake imepewa jukumu la kutekeleza mkakati wa kubidhaisha lugha adhimu ya Taifa Kiswahili ikiwemo kuanzisha madawati ya Kiswahili katika Balozi zinazowakilisha taifa katika nchi mbalimbali duniani, kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7 kila mwaka ambayo imeridhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) pamoja na kuanzisha mashindano ya michezo ya mtaa kwa mtaa yenye lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo na wasanii.
Naye Mwenyekiti za Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amewasisitiza wajumbe wa Baraza hilo kuwa na ushirikiano kati ya watumishi na viongozi wao ili kufikia dhamira ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassani katika kuwahudumia wanachi katika sekta za wizara hiyo.
Aidha, Dkt. Abbasi amesema ili kutekeleza majukumu, maagizo na maekelezo ya viongozi wajumbe wa Baraza na watumishi wanatakiwa kutunza siri za ofisi kwa kufuata Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali inayotolewa na viongozi.
Katika tukio hilo, Mhe. Mchengerwa alizindua Mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara na Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE)
0 Comments