*********************
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye Jiji la Mwanza.
Mhandisi Msenyele anasema kwa kutambua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama inayowakabili wananchi waishio maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Mwanza hususan maeneo ya milimani, Serikali imeipatia MWAUWASA kiasi cha Shilingi Bilioni Moja ili kuboresha hali ya huduma ya maji kwenye maeneo hayo.
“Tunamshukuru Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake wa kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kuhakikisha miradi inatekelezeka. Kupitia hizi fedha tumeweza kuyafikia maeneo matano yaliyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji,” anasema Mhandisi Msenyele
Anasema fedha hizo zimepatikana kupitia programu maalum ya utekelezaji wa miradi kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Mhandisi Msenyele anasema taratibu za kuainisha maeneo yenye changamoto ya maji zilifanyika kwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali za Mitaa, Madiwani, na Wabunge wa Nyamagana na Ilemela.
“Kwa juhudi na ubunifu wa Rais wetu mpendwa, Mhe. Samia Suluhu Hassan tumepata fedha kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo yenye changamoto,” anafafanua Mhandisi Msenyele.
Anayataja maeneo hayo kuwa ni Mlima wa Rada na Nyamhongolo kwa upande wa Wilaya ya Ilemela na kwa upande wa Wilaya ya Nyamagana anasema ni Ihila- Buhongwa, Luchelele-Mnangani na Kambarage.
Akizungumzia uteuzi wa maeneo hayo Mhandisi Msenyele anasema umezingatia hali halisi ya kijiografia kwani maeneo hayo ni ya milimani na kwamba miundombinu ya MWAUWASA iliyokuwepo haikuweza kuyafikishia huduma.
“Mwanza maeneo mengi yapo mlimani mifumo yetu haikuwa na uwezo wa kufika kwenye maeneo haya lakini kupitia hizi fedha tunajenga miradi ambayo inakwenda kuondoa changamoto hiyo,” anasema Mhandisi Msenyele.
Anasema utelekezwaji wa mradi kwa sasa upo asilimia 40 na utakamilika Aprili, 2022.
0 Comments