Ticker

6/recent/ticker-posts

SINGIDA WAANZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA ELIMU KWA WATOTO WADOGO

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Binilith Mahenge akieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana mkoani kwake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Wanafunzi wa darasa la Awali wakifurahia mazingira ya kujifunzia katika darasa jipya lililojengwa hivi karibuni.
Wanafunzi wa darasa la Awali wakiwa katika harakati za kujifunza mambo mapya darasani.


Na Abby Nkungu, Singida

MKOA wa Singida umefanikiwa kuongeza kiwango cha uandikishaji wanafunzi elimu ya awali kwa zaidi ya asilimia tisa kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha sekta hiyo kuanzia ngazi ya chini katika kumwezesha kila mtoto kupata haki ya msingi ya elimu.

Mkuu wa mkoa, Dk Binilith Mahenge alibainisha hayo mjini hapa katika taarifa yake juu ya Mafanikio mbalimbali ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Mahenge alisema kuwa katika kipindi hicho, kiwango cha uandikishaji wanafunzi wa darasa la Awali kimeongezeka kutoka wanafunzi 43,801 sawa na asilimia 87 mwaka jana hadi 49,785 sawa na asilimia 96.6 ya lengo kufikia mwezi Machi mwaka huu.

Alieleza kuwa pamoja na sababu nyingine, kupanda kwa uandikishaji huo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuanzishwa shule shikizi 77 kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huu katika kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Naye Ofisa elimu mkoa wa Singida, Maria Lyimo alifafanua kuwa shule hizo shikizi zina wanafunzi wa chekechea takriban 8,700 ambao wanaendelea na masomo kama kawaida.

“Wewe unajua Singida ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT- MMMAM). Kwetu sisi, hii ni sehemu ya utekelezaji wa Programu hiyo ambayo uzinduzi wake ulifanyika Dodoma mwaka jana” alisema Ofisa elimu huyo.

Mmoja wa walimu katika shule shikizi Mwembe Mmoja nje kidogo ya mji huu, Fatuma Yusufu alisema kuwa shule hizo zimesaidia kupunguza utoro, kuongeza usikivu darasani na kuwafanya watoto kupenda elimu.

“Wapo watoto katika baadhi ya shule wanatoka mbali na wanatembea zaidi ya kilomita 14 kwenda shule na kurudi nyumbani. Hebu fikiria, mtoto wa chini ya miaka minane anayesoma chekekechea anafika shuleni kachoka, anapiga miayo tu kwa njaa na uchovu kisha anachapa usingizi darasani hivyo hasomi chochote" alieleza Mwalimu huyo.

Nao baadhi ya wazazi na walezi wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizosaidia katika ujenzi wa shule hizo shikizi ili kuondoa adha; hasa kwa watoto wanaosoma Chekechea.

“Watu wamekuwa wakijiuliza kwa nini wazazi wengi wanapenda kupeleka watoto wao wadogo shule binafsi za Awali. Sababu ni kama hiyo.....mazingira ya shule zetu nyingi za Serikali hayakuwa rafiki kwa watoto wadogo. Kwa kweli Mama ameupiga mwingi kwenye elimu, sekta hii itapanda sana” alisema Ntandu Mumwi, mkazi wa Utemini.

Rehema Ali mkazi wa Mandewa pamoja na kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za madarasa hayo, alisema bado kuna haja ya kuboreshwa zaidi mazingira; hasa kwa watoto wadogo ambao hupenda michezo mbalimbali jambo ambalo pia linaungwa mkono na Wataalam wa masuala ya watoto.

Tanzania ni Nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuifanya elimu ya Awali kuwa ya lazima kwenye Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili kuijumuisha elimu ya Awali katika elimu ya msingi kwa kuzitaka shule zote za msingi kuwa na darasa la Awali kwa watoto walio chini ya miaka mitano.

Post a Comment

0 Comments