Ticker

6/recent/ticker-posts

VIJANA SINGIDA WAFUNDWA MAADHIMISHO YA 58 YA MUUNGANO


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akizungumza na vijana katika Kongamano la Maadhimisho ya 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika jana Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Uhasibu kwa kuwashirikisha Vijana wa kada mbalimbali.

Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akizungumza kwenye kongamano hilo.
Vijana wakishiriki kongamano hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akisisitiza jambo kwenye kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Kongamano likiendelea.Vijana wakiwa kwenye kongamano hilo

************************

Na Mwandishi Wetu , Singida

VIJANA Mkoa wa Singida wametakiwa kujiamini, kuonesha na kuvitumia vipaji walivyonavyo katika kuleta ubunifu na ugunduzi wa mambo kwa kuwa wengi wana vipaji lakini hawajavitambua.

Hayo yamesema na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge wakati akizungumza na vijana katika Kongamano la Maadhimisho ya 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Uhasibu kwa kuwashirikisha Vijana wa kada mbalimbali.

Muro amewataka vijana kuhakikisha wanatumia akili zaidi kuliko elimu katika kutambua vipaji walivyonavyo na kuchukua hatua.

Akielezea umuhimu wa vijana kutumia akili zaidi kuliko elimu Muro alisema duniani wagunduzi wakubwa hawakutumia elimu lakini walitumia akili na wakafika mbali hivyo kuwataka wajitume na waweze kutumia vipaji vyao kama njia ya kupitisha elimu wanazopata.

Aidha Muro amebainisha kwamba kijana anayemaliza chuo na kukaa mtaani akisubiri Serikali itoe ajira ni matokeo mabaya ya matumizi ya vipaji kwa kuwa kila mmoja amepewa kipaji chake.

Amewataka vijana kujiunga katika vikundi na kuvisajili ili waweze kupata mikopo kupitia asilimia nne katika Halmashauri zao huku akiwakumbusha Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa msaada wa mawazo kwa vijana waliopo wenye vikundi.

Muro ameendelea kusema kwamba huenda matumizi mabaya ya simu janja ndio chanzo cha vijana kushindwa kufikiria vizuri namna ya kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo ugunduzi wa vipaji vyao na namna ya kupata mitaji na utajiri kwa ujumla.

Amewataka vijana kutumia Kongamano kuzitumia fursa ambazo zimekuwa zikioneshwa katika mada mbalimbali zilizowasilishwa, na kila mwenye kipaji kuanza kuzitumia.

Afisa Vijana Mkoa wa Singida na mratibu wa kongamano hilo, Frederick Ndahani alisema lengo la kongamano hilo ni kuonesha fursa za kiuchumi ambazo zimezunguka Mkoa wa Singida ili waweze kuzitumia na kujikwamua katika maisha yao ya kila siku.

Aidha akieleza jitihada za Serikali katika Mkoa wa Singida zakuwainua vijana alisema katika kipindi cha mwaka 2018/2022 Mkoa umetoa jumla ya Sh. Milioni 601.4 ikiwa ni mikopo iliyotolewa katika vikundi 133.

Amebainisha kwamba jumla ya ekari 23418 zimetengwa kwa ajili ya vijana ili kufanya shughuli za uwekezaji na michezo katika Wilaya ya Manyoni Ikungi Singida na Itigi.

Ndahani amewataka vijana kuacha kutumika katika matukio ya uvunjifu wa amani na kujihusisha na mambo ambayo yatawajengea uaminifu katika jamii.

Katika Kongamano hilo Vijana walifundishwa Wajibu wa Vijana katika kuulinda Muungano wa wetu, Fursa za Vijana zinazopatikana katika Mkoa wa Singida, Wajibu wa Vijana katika kushiriki Sensa ya Watu na Makazi pamoja na utaratibu wa kupata mkopo kutoka Halmshauri na mfuko wa maendeleo wa Vijana.

Post a Comment

0 Comments