Ticker

6/recent/ticker-posts

WCF YAZOA TUZO TATU MAADHIMISHO YA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

Mwandishi wetu - DODOMA

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepata tuzo tatu katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambapo kwa Tanzania yamefanyika katika viwanja vya Kituo cha Mikutano Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kilele hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka waajiri na wafanyakazi kuendelea kushirikiana pamoja ili kuweka mzingira yenye usalama na afya katika maeneo ya kazi ikiwemo kuzuia vihatarishi.

Amefafanua kuwa, kuweka mazingira salama kunapunguza gharama kwa sababu wafanyakazi wanapopata ajali au ugonjwa kutokana na kazi inavuruga mipango ya uzalishaji kwa pande zote mbili.

“Waajiri na wafanyakazi ni lazima wafahamu suala la afya na usalama mahali pa kazi ni mkakati wa pamoja na ni sehemu ya utekelezaji wa Mfumo wa haki na wajibu ulioainishwa kimataifa na kanuni ya kuzuia vihatarishi inapewa kipaumbele cha juu zaidi”, alieleza Waziri Ndalichako.

Wakati huohuo, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili kuongeza ufanisi wa kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.

Ahadi hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Shirika hilo, Ndg. Getrude Sima baada ya WCF kushinda tuzo tatu katika maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambapo kwa Tanzania yamefanyika katika viwanja vya Kituo cha Mikutano Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

“Tutaendelea kushirikiana na WCF kupitia mikakati yetu mbalimbali ndani ya Shirika la Kazi Duniani hapa Tanzania kwa hiyo niwapongeze sana na nimefurahi kuona kwamba nanyi pia mmeweza kushiriki na kuwaeleza wananchi mnachofanya,” ameeleza Ndg. Sima.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda ameipongeza WCF kwa kushinda tuzo nyingi zaidi na kuitaka Taasisi hii kuendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.

Akizungumzia maadhimisho haya, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema Mfuko huu umekwisha lipa fidia kwa wafanyakazi mbalimbali waliopata ajali wakiwa kazini na baadhi yao wameshiriki katika Maadhimisho haya.

Kuhusu huduma zilizotolewa amesema WCF imeshirikisha wanufaika wao katika kutoa elimu ya fidia kwa wadau waliotembelea Maadhimisho haya. Pia imeweza kuonesha viungo bandia vinavyolipiwa na WCF kwa wahitaji wa viungo hivyo, pamoja na uwepo wa madaktari tunaoshirikiana nao katika utoaji wa huduma mbalimbali za kitabibu”, amehabarisha Dkt. Omar.

Sambamba na hayo, wanufaika wa Mfuko huo, wameishukuru Serikali kwa kuanzisha WCF ambayo imeweza kuwalipia gharama za matibabu, kuwanunulia viungo bandia ikiwemo miguu na mikono bandia pamoja na kuwalipa pensheni kila mwezi huduma ambayo itaendelea mpaka mwisho wa uhai wao.

“Mbali na pensheni ninayopata kila mwezi, WCF walinililipa fidia ambayo imeniwezesha kununua bajaji na nimejiajiri kama dereva. Nashukuru sana kwani naihudumia familia yangu kama nilivyokuwa kabla ya ajali,” amearifu Ndg. Deus Anthony.

Naye Bw. Hamisi Omari ameshukuru kwa kutibiwa, kununuliwa mkono wa bandia na kuendelea kulipwa pensheni kila mwezi.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umepata tuzo ya Mwajiri Bora katika Sekta za Bima, Hifadhi ya Jamii na Usalama Mahala pa Kazi, tuzo ya Muoneshaji Bora katika kujali Wafanyakazi wenye Mahitaji Maalum na tuzo ya Mshindi wa tatu katika Taratibu za Usimamizi wa Usalama Mahala pa Kazi kwa Sekta ya Umma.

WCF ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa kwa lengo la kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wanaumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako(kushoto), akimkabidhi Meneja Tathmini za Vihatarishi Sehemu za Kazi kutoka WCF, Bi. Naanjela Msangi, Moja ya tuzo hizo



Afisa Mwandamizi Idara ya Tathmini WCF, Bw. Robert Duguza (wakwanza kushoto) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa na WCF

Post a Comment

0 Comments