Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAHIMIZA KAMATI YA BUNGE YA VIWANDA,BIASHARA NA MAZINGIRA KUTANGAZA FURSA KATIKA ENEO HURU LA BIASHARA AFRIKA


*************

SERIKALI kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara yahimiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar walioshiriki warsha ya kujenga uwezo na uelewa wa wadau nchini kuhusu Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA) kutangaza fursa zilizoko katika eneo huru la Biashara Afrika Ili wananchi wajiandae kuzitumia.

Hayo yamesemwa leo tarehe 22 Mei, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Sea Cliff uliopo Zanzibar na Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara alipokuwa akizungumza na Wabunge walioshiriki kwenye warsha hiyo.

Mhe. Kigahe amesema kuwa Wizara yake na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kwa kushirikiana na Sekreteriet ya AfCFTA, Wadau wa Maendeleo GIZ na Benki ya Afrexim ipo katika zoezi endelevu kwa ajili ya kuhabarisha Umma kuhusu Mkataba wa AfCFTA na imeiona ipo haja na umuhimu wa kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge nchini ili kuzijua fursa zilizopo kupitia Mkataba huo.

“Waheshimiwa Wabunge ndio wawakilishi wa wananchi na hivyo watakuwa wasemaji wazuri kuhusu Mkataba wa AfCFTA popote pale watakapokuwa. Hivyo, nawashukuru kwa utayari wenu kuhudhuria warsha hii muhimu” Amesema Mhe. Kigahe.

Ameongeza kuwa Mkataba wa AfCFTA unatoa fursa ya kuwa na soko la pamoja la bidhaa na huduma lenye jumla ya nchi 55 zenye takriban watu Bilioni 1.2 na pato ghafi la taifa lenye jumla ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4 na fursa za uchumi unaokua kwa kasi. Vile vile, utekelezaji wa mkataba huo unatarajiwa kuongeza mchango wa biashara wa Afrika kwenye soko la dunia kwa asilimia 2.8 huku sekta za kilimo, chakula na huduma zikipewa nafasi kubwa katika ukuaji huo.

Akifungua Warsha hiyo Mgeni rasmi Mhe. Omar Said Shabaan Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amefurahishwa na ujio wa Sekretariati AfCFTA iliyopo Accra, Ghana kwa kuratibu makongamano haya ya kujenga uwezo ili kuweza kutumia fursa zitokanazo na soko hilo miongoni mwa Nchi Wanachama.

Mhe. Shaaban amewapongeza Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamefika kushiriki katika warsha hiyo ambayo ni maalum kwa lengo la kuhabarishana na kupeana uelewa zaidi kuhusu Mkataba wa AfCFTA ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sehemu ya Mkataba huo.

Aidha ameishukuru Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Makatibu wa Kamati zote za Bunge kwa namna walivyoshirikiana katika maandalizi ya warsha hii muhimu na kuishukuru Taasisi ya GIZ na Benki ya AFREXIM kwa kukubali kufadhili warsha hiyo ambayo inawalenga haswa Waheshimiwa Wabunge kutoka Kamati mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya Biashara na Uwekezaji kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

“Mkataba wa AfCFTA ulitiwa saini katika Mkutano wa 10 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika tarehe 21 Machi 2018 Kigali nchini Rwanda na mnamo tarehe 9 Septemba 2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio na Kurudihia Mkataba huo na Serikali iliwasilisha rasmi Hati ya Kuridhia (Instrument of Ratification) mnamo tarehe 17 Januari 2022 katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama kamili wa Mkataba huo na ina haki na wajibu katika kunufaika na fursa zilizoainishwa na zitakazojitokeza katika utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA.” Amesema Mhe. Shaaban.

Semina hii imehudhuriwa na Waheshimiwa Mawaziri kutoka Tanzania bara na Zanzibar, Makatibu wakuu kutoka Tanzania bara na Zanzibar, Waheshimiwa Wabunge wa kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Waheshimiwa wabunge kutoka Zanzibar, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Sekreterieti ya AfCFTA, Washirika wa Maendeleo GIZ na AFREXIM Bank, Wakurugenzi na Maafisa mbalimbali wa Serikali.

Post a Comment

0 Comments