Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA BILIONI 100 KULETA AHUENI KWA BEI ZA MAFUTA NCHINI


*******************

Na Dotto Kwilasa,DODOMA

SERIKALI imetopa ruzuku ya Shilingi bilioni 100 kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa ajili ya kuleta ahueni katika bei ya nishati ya mafuta nchini.

Hatua hiyo inatokana na mahitaji ya wananchi, maoni na ushauri wa Wabunge, maelekezo ya Chama cha Mapinduzi na kupelekea Rais Samia kutoa maelekezo kwamba ahueni ya bei ya mafuta itafutwe mapema badala ya kusubiri mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema hayo leo wakati akiwasilisha bungeni taarifa ya Serikali kuhusu hatua za dharura za kupunguza bei ya nishati ya mafuta.

Akieleza hayo Waziri Makamba amesema "Hivyo basi, kama hatua ya dharura, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwamba, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh. 100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini,"amesema na kuongeza;

“Ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22,aidha kutolewa kwa ruzuku hiyo hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea,"anaeleza Mbali na ruzuku hiyo,Waziri huyo wa Nishati amesema nafuu nyingine itaanza mwaka ujao wa fedha kutokana na hatua ya Serikali kuomba mkopo kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

“Mchakato wa kuchukua mkopo huo uko mbioni kukamilika na ahueni kwenye kupanda kwa bei za bidhaa itapatikana katika mwaka ujao wa fedha,” amesema

Amezitaja hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali kuwa ni pamoja na kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo na kwamba Wizara imekamilisha kufanya tathmini ya kampuni zote zilizoonesha nia ya kuweza kuleta mafuta kwa bei nafuu kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wao wa kuleta mafuta hayo ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini unakuwa sio wa kusuasua.

"Mipango hii ikileta matokeo yanayotarajiwa, bei za mafuta zitapungua zaidi kuanzia mwezi Agosti 2022, Serikali pia itaanzisha Mfuko wa kuhimili Ukali wa Bei za mafuta na imeandaa utaratibu wa kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kupunguza makali ya bei ya mafuta kipindi ambacho bei hizo zinaongezeka kwa kiasi kikubwa,"amefafanua

Mpango mwingine ni kuanzisha hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve) ambapo Serikali inakamilisha marekebisho ya Kanuni za kuanzisha na kuendesha hifadhi mafuta ya kimkakati ili nchi ijihakikishie usalama wa upatikanaji wa mafuta na unafuu wa bei katika vipindi kama hivi.

"Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa na kituo kikubwa cha mafuta ,kwa sasa inakamilisha makubaliano ya kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya kuuzwa ndani na nje ya nchi kulingana na uhitaji,uwepo wa kituo hiki utawezesha nchi kupata mafuta yenye bei nafuu pale bei zinapopanda kupita kiasi ambapo mpango huu na utekelezaji wake unaweza kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu,"amesema

Post a Comment

0 Comments