Ticker

6/recent/ticker-posts

THE ROYAL TOUR YALETA MAFANIKIO, HOTELI ZA KITALII NDANI YA MIKOA MITATU ZAJAA KWA YA MIEZI MITATU.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dr. Ashatu Kijaji akikagua kwenye banda la maonesho la Wakala wa Usajili wa biashara (BRELA) kabla ya kuzindua maonesho ya 9 ya biashara na utalii jijini Tanga.
Dr. Ashatu Kijaji akiongea na baada ya ukaguzi wa banda hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima aakifafanua jambo kwa Waziri wakati wakiendelea na ukaguzi.

*********

Na Hamida Kamchalla, Tanga.

Mafanikio ya The Royal Tours yameanza kuonekana katika Mikoa mitatu nchini ambapo wamiliki wa hoteli kubwa na nyumba za kulala wageni zote za kitalii wamenufaika kwa kuuza vyumba vyote ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Hayo ameyasema Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dr. Ashatu Kijaji wakati akizindua maonesho ya 9 ya biashara na utalii Mkoa wa Tanga ambapo alifafanua kwamba mahoteli katika Mikoa ya Daresalaam, Arusha na Kilimanjaro yamejaa kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo kutokana na filamu ya Royal tour aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hasan ya kuhamasisha utalii nchini.

Aidha amewataka wafanyabiashara mkoani Tanga kuchangamkia fursa za watalii wanaoingia nchini kwa kutoa huduma zenye viwango vinavyohitajika kwani wageni wengi wanakuja nchini baada ya kuvutiwa na filamu hiyo iliyofanywa hivi karibuni.

Dr. Kijaji pia ametoa rai kwa Watanzania kujipanga kikamilifu katika kuchangamkia fursa, mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga hoteli nzuri zenye viwango kwajili ya malazi ya watalii, wawekezaji na wafanyabiashara ndani ya Taifa huku akiitaka jamii kujiandaa kwa pamoja kwajili ya kupokea watalii nchini.

“Hoteli zote kubwa za kitalii zimejaa kwa miezi mitatu ijayo, hivyo nimewaambia umoja wa mahoteli hapa Tanga mnaposikia majirani zenu wote hawana nafasi ya kuhudumia kilichobaki mbele yako ni wewe kujipanga vizuri hususani katika hili jiji la Tanga na mahoteli yake kupokea watalii na wawekezaji, “alisisitiza waziri Kijaji.

Aidha Waziri huyo amewataka wafanyabiashara kujipanga kikamilifu kuhakikisha huduma wanazotoa zinatoka kwa kiwango kinachokubalika na kujua bidhaa wanazouza ni za kiwango gani na kwamba Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao wamejiandaa vizuri kuona wanashirikishana kwenye fursa hizo ili waandae mazingira ambayo ni wezeshi kwa kuelezana yale yote yanayohitajika na hatimaye waweze kunufaika na fursa hizo zilizoletwa na Rais kupitia filamu ya the Royal tour.

"Lengo la kufanya hivyo ni kuona uchumi wetu kupitia biashara na utalii unakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa, takwimu zinaonyesha uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa pato la Taifa nchini umeongezeka na kufikia asilimia 35, jambo ambalo limeonesha mwamko mkubwa" alibainisha.

Hivyo Dr. Kijaji amebainisha kwamba kupitia maonyesho hayo alimuahidi Rais kuwa ndani ya miaka yake mitatu kwenye uongozi wake wa awamu ya kwanza kuwa wanataka wafikie nchini China ikiwezekana wawapite kwakuwa Taifa letu lina vivutio vingi na fursa nyingi za uwekezaji.

“Katika kufikia hayo, serikali imefanya tumeweza kuridhia mkataba wa eneo huru la biashara la Afrika, ndani ya soko huru hili la Afrika timeingia mkataba wa kwenda kuuza bidhaa zetu kwenye nchi 54 na sisi tukiwa wa 55" alibainisha waziri huyo.

Naye mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amesema kuwa lengo la maonyesho hayo ya tisa ni kutoa elimu ya biashara na ujasiriamali kwa wafanyabiashara ndani ya Mkoa wa Tanga.

“Nikuambie tu wazi mheshimiwa Waziri, Tanga tuna tabia ya kutojithamini sisi wenyewe, mwaka jana yale makampuni makubwa ambayo hayakushiriki tumeburuzana kwa nguvu na yameweza kushiriki kikamilifu mwaka huu nimesema wazi kabisa haya makampuni makubwa ambayo hayataki kukaa na kushiriki katika maonesho haya lakini biashara zao na pesa zao wanapata kupitia Tanga basi wasiwe sehemu ya ofisi yangu, “alisistiza Malima.

Post a Comment

0 Comments