Ticker

6/recent/ticker-posts

BIDHAA ZA CHAKULA NA MBOGAMBOGA ZINAZOKWENDA ZANZIBAR HAZITOZWI KODI


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande akijibu swali Bungeni jijini Dodoma.

***************

Na Farida Ramadhani, WFM

Serikali imeeleza kuwa bidhaa za chakula na mbogamboga halisi zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar hazitozwi kodi, tozo na ushuru wa aina yoyote kwa mujibu wa sheria.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chaani, Mhe. Usonge Hamad Juma, aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kupunguza kodi, tozo na ushuru wa bidhaa za chakula na mbogamboga kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ili kudhibiti mfumuko wa bei wa bidhaa hizo.

Mhe. Chande alisema kuwa bidhaa hizo hazitozwi tozo ya uchakataji nyaraka kwa sababu hazihitaji kufanyiwa mchakato wa nyaraka katika mfumo wa forodha.

Alisema bidhaa za chakula zinazotozwa tozo ni zile zinazotoka viwandani ambazo hutozwa tozo ya uchakataji nyaraka za forodha ya asilimia 0.6 tu kwenye thamani ya mzigo huo.

“Lengo la tozo hii ni kugharamia huduma ya uchakataji wa nyaraka za forodha na hutozwa kwa wateja wote wanaotumia Mfumo wa Forodha (TANCIS)”, alibainisha Mhe. Chande.

Wakati huohuo, Mhe. Chande alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kiukaguzi wa miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya kimataifa kwa lengo la kuzuia upotevu wa mapato.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina alijetaka kujua namna ambavyo Serikali imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma kati ya makampuni ya kimataifa.

Alisema hatua hizo ni pamoja na kuendelea kuboresha mifumo ya ndani ya ukusanyaji kodi kama vile Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Utoaji wa Risiti za Kielektroniki na Mfumo wa Kuwasilisha Ritani Kielektroniki.

“Kutoa mafunzo ya vitendo kwa watumishi katika nchi mbalimbali zenye uzoefu wa kushughulikia miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni za kimataifa”aliongeza Mhe. Chande.

Alisema kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa kubadilishana taarifa kati ya Serikali ya Tanzania na nchi zingine pamoja na kuendelea kufanya majadiliano na wadau mbalimbali ili kuona uwezekano wa kujiunga na Global Forum on Tax Transparency na ubadilishanaji wa taarifa kwa lengo la kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa pia ni miongoni mwa hatua hizo.

Post a Comment

0 Comments