Ticker

6/recent/ticker-posts

SIKU YA BAHARI DUNIANI: UDSM YAHAMASISHA JAMII KUTUNZA FUKWE ZA BAHARI DHIDI YA TAKA NGUMU KWA KUFANYA USAFI

Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wadau mbalimbali wa Mazingira wakifanya usafi katika fukwe za bahari kwenye soko la Samaki Kunduchi Jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha Siku ya Bahari Duniani leo Juni 8,2022. Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wadau mbalimbali wa Mazingira wakifanya usafi katika fukwe za bahari kwenye soko la Samaki Kunduchi Jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha Siku ya Bahari Duniani leo Juni 8,2022. Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wadau mbalimbali wa Mazingira wakipata picha ya pamoja mara baada ya kufanya usafi katika fukwe za bahari kwenye soko la Samaki Kunduchi Jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha Siku ya Bahari Duniani leo juni 8,2022

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

*************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Shule Kuu ya Sayansi Akua na Teknolojia ya Uvuvi kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi wameadhimisha Siku ya Bahari Duniani kwa kufanya usafi katika fukwe za bahari Kunduchi Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wanafanya zoezi hilo leo Juni 8,2022, Amid Shule Kuu ya Sayansi Akua na Teknolojia ya Uvuvi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt.Brandina Lugendo amesema wao kama waandaaji wa zoezi hilo pamoja na jumuiya ya wahitimu wameona waadhimishe siku hii kwa kufanya usafi maeneo ya Pwani hasa kuondoa taka ngumu kwasababu taka ngumu zimekuwa ni tatizo katika ukanda wa bahari.

Amesema lengo lao ni kuhamasisha uelewa kwa wananchi wa kawaida lakini pia kwa wanafunzi na wahitimu ili kujua jinsi ya kutunza taka na kuondokana na tatizo uchafu wa taka ngumu kwenye mazingira ya bahari.

"Taka ngumu zimekuwa na athari nyingi za kimazingira zikiwemo kuathiri viumbe vya baharini hasa wale ambao wanaziona kama chakula na kuwafanya wasiweze kuishi pia tatizo hili linasababisha kuharibu madhari na kuondoa kivutio kwa watalii katika maeneo ya Pwani". Amesema Dkt.Lugendo.

Nae Mratibu wa Jumuiya ya Wahitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bw.Daniel Steven amesema wamewakutanisha wahitimu wao na kufanya kazi mbalimbali ambazo zinamanufaa katika jamii kama zoezi hilo ambalo wamelifanya la kusafisha fukwe za bahari ya Hindi katika soko la samaki Kunduchi.

Amesema kattika zoezi hilo la kufanya usafi katika fukwe za bahari wanahakikisha wanaondoa taka ambazo haziozi ambazo zimekuwa zikichafua kwa kiasi kikubwa mazingira na kuleta athari kwa vizazi vya samaki kwenye bahari.

Pamoja na hayo amehimiza jamii kuendelea na utunzaji wa mazingira na kuangalia namna ya kuyaweka safi kwani sasa hivi kuna tatizo la mabadiliko ya Tabia nchi kwahiyo kunahitajika kuwepo kwa uelewa mkubwa wa utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Afisa Uvuvi Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Ambakisye Semtoe amesema wameshiriki zoezi hilo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha shughuli za usafishaji wa mazingira na kujizuia utupaji taka kwenye vyanzo vya maji nchini.

Ameeleza kuwa kunahitajika jjitihada za makususdi kuhakikisha kwamba tunazuia utpaji taka baharini lakini pale zikiwa zimeshatupwa kunakuwepo na juhudi za kusafisha mazingira.

Ametoa wito kwa watumiaji wa bahari kujizuia kutupa taka baharini na wawe na mifumo ambayo baada ya kutumia vittu mbalimbali ambavyo vinazalisha taka hasa taka ngumu zisizooza basi wawe wanarudi nazo nchi kavu kwaajili ya kutupwa katika maeneo husika.

"Niwaombe watendaji walioko karibu na fukwe za bahari wawahamasishe wananchi kwenye ukusanyaji wa taka ngumu na kuzuia utupaji wa taka katika maeneo ya bahari kwani taka hizo ni hatari kwa viumbe mbalimbali wanaopatikana ndani ya bahari". Amesema



Post a Comment

0 Comments