Ticker

6/recent/ticker-posts

MIKAKATI ENDELEVU YA KUIMARISHA UHURU WA KUJIELEZA NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NCHINI TANZANIA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
**
Uhuru wa kujieleza/kutoa maoni ni suala mtambuka linaloigusa jamii nzima. Bahati mbaya bado kuna mtazamo potofu kwamba utetezi wa uhuru wa kujieleza unawahusu wanahabari na wadau wa habari pekee.

 Mtazamo huu umechangia kufifisha harakati za utetezi wa uimarishaji wa mazingira yanayolinda na kuimarisha misingi ya uhuru wa kujieleza na kupata habari hapa nchini.

Ieleweke kwamba, uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi inayolindwa na Sheria Mama, yaani, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haki hii pamoja na haki nyingine zikiwemo haki ya kuishi na kufanya kazi, haki ya kuabudu, kukusanyika, kushiriki siasa, n.k. ni mojawapo wa misingi ya haki za binadamu.
 Kuingiliwa kwa uhuru huu hupelekea wananchi kuwa wasindikizaji katika michakato mbalimbali ya maendeleo. Mfano, uhuru wa kutoa maoni ndio humuwezesha mwananchi kuhoji mapato na matumizi ya Serikali, kuhoji ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka na kupongeza jitihada za Serikali za kuleta maendeleo.

 Bahati mbaya, uhuru huu unaathiriwa na utekelezaji wa sheria zinakandamiza watu na/au vyombo vya habari kuitumia haki hii ya kikatiba.

Kwa muda mrefu wanahabari na wadau wa habari wamekuwa mstari wa mbele kudai mazingira bora ya kisheria na kisera ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza nchini. Ni wakati sasa wa wananchi kujitokeza kuunga mkono jitihada hizi. 

Watanzania washiriki kuihimiza serikali na wadau mbalimbali kuboresha mazingira ya uhuru wa kujieleza na kupata taarifa, ikiwemo ulinzi wa faragha na usalama wa taarifa binafsi.

Athari za udukuzi wa taarifa binafsi na uvamizi wa faragha za mtu binafsi unaotokana na maendeleo ya kidigiti na teknolojia ya habari na mawasiliano unahitaji kudhibitiwa kwa sheria zitakazowalinda raia dhidi ya wadukuzi.

Vyombo vya habari viwahimize wananchi kushiriki katika mchakato unaoendelea wa kurekebisha Sheria ya Huduma ya Habari ya 2016 kwa kutoa maoni yao ili kupata sheria bora itakayoimarisha utoaji na upataji taarifa kupitia vyombo vya habari. 

Aidha, wananchi washiriki kuihimiza Serikali na wadau wa habari kuzifanyia mapitio na marekebisho sheria zote zinazoathiri haki ya kujieleza.


Mkakati mwingine ni kuimarisha utoajie wa elimu ya uhuru wa kujieleza kupitia mitaala ya vyuo vya kati na vikuu vya Uandishi wa habari na mawasiliano hapa nchini. 

Pia, jitihada zielekezwe katika uanzishwaji wa Klabu zinazofanya utetezi na uhamasishaji uhuru wa kujieleza katika vyuo vya uandishi wa habari kama njia mojawapo ya kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na uelewa mpana kinadharia na kivitendo.

Post a Comment

0 Comments