Ticker

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI 3 MKOANI TANGA ZIMEKABIDHIWA AFUA YA UNYUNYIZIAJI VIUADUDU VYA KIBAIOLOJIA KWENYE MAZALIA YA MBU***************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MAPAMBANO dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini yanahitaji ushiriki wa kila mtu ili kuweza kufikia lengo la Kitaifa la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa afua ya unyunyiziaji viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu ambapo alitoa wito wa wadau kujitokeza kuwezesha utekelezaji wa mpango huo na kaulimbiu yake ni, 'zero malaria 2030 inawezekana na inaanza na mimi'.

Mwalimu alisema Wizara yake imeandaa miongozo na kanuni za utekelezaji, ili kuhakikisha afua hiyo inatekelezwa kwa ubora unaostahili, hivyo ni muhimu kuainisha katika halmashauri ambazo zikiitekeleza italeta tija na kuchangia katika kufikia lengo hilo.

"Naelekeza Wizara kuchapisha na kusambazwa miongozo na kanuni za utekelezaji wa afua hii, pamoja na kufanya mafunzo kwa halmashauri 176 zilizobaki, ili kurahisisha upatikanaji wa viuadudu kote nchini, natoa wito kwa uongozi wa kiwanda cha kutengeneza viuadudu hivi, kuweka mawakala katika Mikoa yote" amesema.

Aidha alifafanua kwamba, jumla ya lita 16, 980 za viuadudu vya kibaiolojia zenye thamani ya sh milioni 224 zimenunuliwa na kusambazwa katika halmashauri 3 za Tanga jiji, Handeni na Lushoto kwa Kuzingatia ukubwa wa mazalia yaliyopo.

"Viuadudu hivyo vinatumika wakati wa mzunguuko wa kwanza ambao ulianza mwezi juni, na unatarajiwa kukamilika julai 29 mwaka huu, lakini pia jumla ya pampu 632 zenye thamani ya sh milioni 21,280 zimenunuliwa na kukabidhiwa halmashauri zinazotekel eza atua hii.

"Naelekeza kuwa, vifaa hivi vitumike vizuri na kwa kuzingatia madhumuni yaliyokusudiwa ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa, ninatoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwezesha utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji viuadudu katika halmashauri nyingine hapa nchini" amebainisha.

Hata hivyo Waziri huyo alibainisha kwamba ugonjwa wa malaria bado ni tatizo nchini, hivyo serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau mbalimbali imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini kutoka zaidi ya asilimia 50 mwanzoni mwa miaka ya 90 hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2017.

"Kwa sasa, Wizara kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria inatekelezwa mpango mkakati wa malaria wa miaka mitano (2021 - 2025) unaolenga kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7.5 mwaka 2017 hadi kufikia chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025" amesema.

"Mpango mkakati huu umebeba mikakati sita ambayo ni kutoa huduma za vipimo, matibabu na tibakinga kwa wagonjwa wa malaria, kufanya tathimini na ufuatiliaji, kuhakikisha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za malaria kwenye vituo, kufanya uhamasishaji wa jamii kuhusu afya za malaria pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha na watumishi wenye sifa ili kuweza kutekeleza afua mbalimbali za malaria kwa ufanisi" amefafanua.

Naye Balozi wa Uswisi nchini Didier Chassot alisema mradi huo uliozinduliwa wanapenda kuiona Tanzania isiyo na malaria na wanaamini inawezekana hivyo mradi umepewa kiasi cha sh bilioni 14 kufanya kazi na Wizara ya Afya bega kwa bega.

"Leo tuko hapa kuzindua afua mpya kupambana na ugonjwa wa malaria, afua ya kumwagilia viuadudu kwenye mazalia ya mbu, malaria inazuilika ila ni lazima sote tutimize wajibu wetu na tuna nafasi katika hilo, na kwenye jamii, wananchi inabidi tutunze mazingira yetu kupunguza mbu" amesema.

Aidha alibainisha kwamba wawakilishi wa wananchi bungeni wanapaswa kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha, kuweka mazingira mazuri kisheria, kutetea afua pamoja na kuhimiza uwazi na uwajibikaji huku alisisitiza kuwa nchi ya Uswisi itaendelea kushikana na Tanzania katika kutokomeza malaria.

Jumla ya halmashauri 3 mkoani Tanga zimekabidhiwa afua ya unyunyiziaji viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu, ambayo imefadhiliwa na serikali ya Uswisi kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo (SDC) kwa kufadhili utekelezaji wa afua hiyo pamoja na misaada mingine ambayo inatoa ili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya malaria.

Post a Comment

0 Comments