Ticker

6/recent/ticker-posts

MLALO FC BINGWA SHANGAZI MLALO JIMBO CUP 2022

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (kulia) akikabidhi kombe kwa timu ya Mlalo FC ambayo imeibuka kidedea kwenye fainali za Shangazi Mlalo Jimbo Cup kwa goli 1-0 dhidi ya timu ya Shume FC Julai 16, 2022 iliyofanyika Mlalo wilayani ya Lushoto mkoa wa Tanga. Kushoto ni Mbunge wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (kulia) akisalimiana na Mbunge wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi (kushoto) mara baada ya kuwasili Mlalo kwa hafla ya kufunga mashindano ya Shangazi Mlalo Jimbo Julai 16, 2022 Mlalo wilayani ya Lushoto mkoa wa Tanga.


Mbunge wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi (wa saba kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalist Lazaro (wa sita kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya Shume FC kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali za Shangazi Mlalo Jimbo Julai 16, 2022 ulichezwa Mlalo wilayani ya Lushoto mkoa wa Tanga.

************************

Na Eleuteri Mangi, WUSM- Lushoto

Timu ya Mlalo FC imeibuka kidedea kwa goli 1-0 dhidi ya timu ya Shume FC zote za Mlalo Wilayani Lushoto mkoa wa Tanga katika fainali ya mashindano ya ligi ya Shangazi Mlalo Jimbo Cup.

Akifunga mashindano hayo Julai 16, 2022 yaliyofanyika Mlalo wilayani Lushoto, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sekta ya michezo nchini kwa kufanya mabadiliko makubwa katika miundombinu ya michezo nchini.

“Kuna mabadiliko makubwa sana katika michezo nchini, tumeanza kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo, kwenye nyasi bandia, tutashuka kwenye jezi na mipira. Kubwa zaidi wizara yetu inakuja na program ya “Mtaa kwa Mtaa” chini ya Waziri wetu Mhe, Mohamed Mchengerwa ambaye Mama amemwamini” amesema Naibu Waziri Gekul.

Mhe. Gekul amesema progamu hiyo itaibua vipaji kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa na kuwahakikishia Watanzania kuwa Mhe. Rais Samia ameagiza, hivyo kama Wizara yenye dhamana ya Michezo nchini hawapendi kushiriki kwenye michezo, wanahitaji ushindi.

Aidha, Naibu Waziri Gekul amempongeza Mbunge huyo kwa kuanzisha ligi ya wanawake huku akishuhudia juhudi kubwa zinazofanywa na timu za wanawake nchini ambao wamelitoa taifa kimasomaso ambapo Timu wa Wanawake chini ya mika 17 Serengeti Girls wamefuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka huu nchini India.

Naibu Waziri Gekul ametumia fursa hiyo kuwaasa watoto wa kike kujihusisha na michezo kwa kuwa Serikali inawekeza kwenye michezo na vipaji vyao vitaonekana na hatimaye kupata ajira hatua itakayowasaidia kuboresha na kuimarisha maisha na uchumi wao.

Ameongeza kuwa wana Mlalo wanajituma katika kujenga taifa kwa kuwa siyo wavivu wanafanya kazi, mazingira ni mazuri na wanamuunga mkono Mhe. Rais katika sekta ya michezo na vijana wana vipaji vya michezo na kusisitiza fainali hiyo imekuwa na mchezo mzuri wa kuvutia kutazama kutokana na vipaji vya vijana ambavyo vitawafikisha mbali kwenye mchezo wa soka.

Ligi ya Shangazi Mlalo Jimbo Cup ya wilayani Lushoto ilianza kurindima Agosti 2021 kwa udhamini wa Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashid Shangazi ambapo mshindi wa kwanza amekabidhiwa kombe na kitita cha Sh. 1,000,000/= na medali kwa kila mchezaji na benchi la ufundi huku mshindi wa pili akijizolea kitita cha Sh. 500,000/= na medali kwa kila mchezaji na benchi la ufundi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashid Shangazi amemshukuru Naibu Waziri Gekul kwa kukubali kwenda kufunga mashindano hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuanzisha mashindano mapya ambayo yatahusisha wilaya nzima ya Lushoto kwa michezo ya mpira wa miguu.

Mbunge huyo amesema kuwa kwa upande wa Jimbo la Mlalo mashindano yatashirikisha mpira wa miguu kwa mabinti, netiboli na mpira wa kikapu na kuongeza kuwa mashindano hayo tayari yamepata mdhamini ambaye ni Kampuni ya Coca cola ambao watatoa vifaa vyote vinavyohusika katika michezo hiyo.

“Kipekee sisi kwetu michezo ni furaha,ni sehemu ya hamasa na pia ni sehemu ya kusambaza matamko mbalimbali ya Serikali, kama ambavyo leo hapa kuna zoezi la kuchanja dhidi ya UVIKO-19 ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono Mhe. Rais ambaye amekuwa mfano na ameendelea kutuasa Watanzania kujilida na ugonjwa huo” amesema Mhe. Shangazi.

Katika fainali hizo pia Zoezi la Sensa ya Watu na Mkazi itayofanyika nchini Agosti 23, 2022 ambapo mashindano hayo yametumika kuwahamashisha watu kushiriki zoezi hilo kwa kuwa maendeleo ya kweli yatafikiwa ikiwa kila mtu atahesabiwa hatua inayosaidia Serikali kupanga mipango endelevu kwa manufaa wa wananchi wake na taifa kwa ujumla.

Fainali hiyo pia imeshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalist Lazaro ambapo ligi ya Shangazi Mlalo Jimbo Cup ilianza kurindima Agosti 2021 kuanzia ngazi ya kitongoji ambavyo vipo 599, vijiji 78, kata 18 na tarafa 3 ambazo zinaunda jimbo la Mlalo likiongozwa na Mbunge Rashid Shangazi.

Post a Comment

0 Comments